Vitu muhimu kwenye maisha vinakuja kwa tatu. Maisha yenyewe yanakuja mara moja tu
Kwanini kufikiria kuhusu kifo husaidia kuishi kwa makusudi na kwa ubora
Wiki iliyopita kwenye watushule.com nilizungumzia kuhusu vitu muhimu vya maisha huonekana kuja kwa tatu. Na tukafikia muafaka kuwa mahusiano, afya na kazi ndio vitu muhimu zaidi kwenye maisha.
Na nilitoa ahadi kuwa siku zinazofuata nitaelezea kwa undani ni vitu gani ndani ya mahusiano, afya na kazi ni muhimu pia. Lakini kabla sijafikia huko nimeona umuhimu wa kuzungumzia kitu ambacho watu wengi hatupendi kusikia lakini kitatokea kwenye maisha yetu.
Mahusiano, afya na kazi ni muhimu kwenye maisha lakini sio kwa usawa wala kwa wakati mmoja.
Utotoni mahusiano ni kila kitu, familia na ndugu zetu ndio dunia yetu. Maisha yetu yote tunakuwa tunawategemea wao. Tukiwa watu wazima mahusiano yanapungua na kuisha kwa wengi, na nguvu nyingi inakuwa kwenye kazi. Na uzeeni kila kitu kinategemea afya.
Kitu kikubwa kinachobadilisha hivyo vyote ni muda. Muda ndio unafanya kitu gani kiwe muhimu na wakati gani. Na kitu kikubwa kuhusu muda ni kuwa una mwisho wake. Tulisema kuwa maisha yana mwanzo, kati na mwisho. Binadamu wanazaliwa, wanaishi, na wanakufa.
Hatukuwa na maamuzi ya kuzaliwa kwetu, hatuna maamuzi ya kufa kwetu. Tunaweza kufanya maamuzi ya mahusiano, afya na kazi kwa muda mfupi tunaopewa duniani.
Haijalishi dini, kabila, elimu, mahusiano, afya na kazi yako, wote tutakufa. Na hakuna anayejua atakufa lini, kwa njia ipi, akiwa wapi na anafanya nini basi ni muhimu kutafakari kwa umakini kuhusu hilo na kuishi maisha yetu tukitambua uhalisia.
Haijalishi kama utajua dhumuni lako la kuwa hai duniani au hautajua, ukifika muda wako kifo kitakutembelea.
Haijalishi kama unakubali dhumuni la kuwa hai duniani ni kutokana na maelezo ya dini au wanasayansi, ukifika muda wako kifo kitakutembelea.
Sikukumbushi kuhusu kifo ili uogope, nakukumbusha ili uanze kuishi.
Ukiweza kujua kwamba uhai wako unaweza kutoka sekunde yeyote baada ya kumaliza kusoma hii, itabidi ukae chini na kutafakari namna bora ya kuishi maisha yako.
Haujui siku wala saa ya kuondoka sasa kwanini unahairisha kufuata ndoto zako? Kwanini unakuwa na kiburi na dharau? Kwanini unaumia watu wasipoelewa ndoto na malengo yako? Kwanini una mkasirikia mtu ambaye pengine ndo ikawa mara ya mwisho kuwasiliana?
Steve Jobs, muanzilishi wa kampuni ya Apple, watengenezaji wa simu za iPhone aliongea vizuri sana namna ambavyo kifo kinamsaidia kuishi vizuri, alisema :
“Nilivyokuwa na miaka 17, nilisoma kitu kinachosema “Ukiishi kila siku kama ni siku yako ya mwisho, kuna siku utakuwa sahihi na itakuwa siku ya mwisho.” Ikanivutia sana kwa sababu ni kweli. Kuanzia pale mpaka leo miaka 33 mbele, kila asubuhi nilikuwa najiangalia kwenye kioo na kujiuliza “ kama leo ingekuwa siku yangu ya mwisho kuwa duniani, ningependa kufanya ninachotaka kukifanya? Nikiona jibu ni hapana kwa siku chache mfululizo najua ni muda wa kufanya mabadiliko “
Sasa hive Steve Jobs ni marehemu, lakini aliishi maisha yake na mchango wake kwa dunia hautasahaulika. Mimi naandika ujumbe Hulu kupitia simu ambayo aliitengenezea musings wa kugunduliwa.
Na mimi nimepoteza watu wa karibu wengi sana ndani ya miaka kumi iliyopita. Ukiachana na kifo cha baba yangu, vifo vya marafiki zangu ambao tulikuwa tunalingana umri viliuma zaidi. Na bado vinaniuma sana.
Rafiki yangu wa kwanza alifariki akiwa usingizini. Kwa miaka mingi niliyomfahamu sikuwahi kusikia anaumwa au ana shida za kiafya za kufanya afariki usingizini. Rafiki yangu alikuwa na mtoto mdogo na alikuwa na malengo ya kufunga ndoa, malengo hayakutimia.
Kila nikienda kulala usiku huwa nafikiria kuwa na mimi naweza nisiamke asubuhi.
Rafiki yangu wa pili alikuwa mfanyabiashara anayepambana sana. Alikuwa na ofisi yake maeneo ya chuo kikuu. Siku moja kafika kazini akawa analalamika njaa ina muuma sana ingawa amekula. Watu wakawa wanacheka na kumtania. Akaagiza chakula tena na akashindwa kula, jioni akalalamika zaidi maumivu ya tumbo. Usiku alipelekwa hospitali na mke wake, akafariki asubuhi yake.
Kila nikisikia njaa baada ya kula napata hofu pengine ni shida kubwa ya kupelekea kifo pia kama rafiki yangu.
Mwanzoni nilikuwa naumia, nalia, na kupata hofu kila nikikumbuka kifo. Marafiki zangu tunaolingana umri wamefariki kwa vitu ambavyo hata mimi vingeweza kunitokea muda wowote. Ilinibidi nikae chini na kutafuta funzo kwenye maumivu yangu.
Nikagundua kifo kipo duniani ili kutukumbusha ufupi wa maisha. Kifo ni hamasa kubwa zaidi kwa viumbe hai vyote, kwa kutambua kuwa utakufa itabidi uishi kwa kusudio lako. Haijalishi kusudio lako ni la kidini, kisayansi au kipagani.
Una muda mchache wa kuwa hai, leo au kesho inaweza kuwa siku yako ya mwisho. Swali ni jee, unatumiaje muda mchache uliokuwa nao. Wewe ni kama mimi, umepoteza marafiki na ndugu wenye umri, rangi, afya na mawazo kama yako au bora kushinda wewe.
Kukumbuka kifo isiwe swala la huzuni, inabidi iwe swala la kukuhamasisha uishi maisha yako. Fuata ndoto zako, penda ndugu na marafiki, cheka kwa sauti, jifunze vitu na ishi maisha yako.
Dhumuni kuu la kuwa hai duniani ni kuishi, na kifo ni ukumbusho bora kabisa.
Siku zinazofuata tutaendelea kuangalia kwa undani vitu muhimu vitatu vya kwenye maisha, mahusiano, afya na kazi, na ni muhimu kuvizingatia vitu hivi tukiwa tunatambua kuwa tutakufa.
Hamasa ya kujua kuwa muda wako duniani ni mchache inakuwa ni sawa na petroli inayohitajika kulifanya gari la maisha yako liende. Kwa njia tofauti na muda tofauti tafuta njia za kujikumbusha kuwa maisha yako yana mwisho.
Shiriki kwenye misiba ya watu, tembelea makaburi ya watu wako waliotangulia, soma na fuatilia kuhusu historia za watu waliofariki. Na hii isikufanye uogope au kukata tamaa ya maisha, bali ikupe hamasa ya kufuata ndoto na malengo yako.
Wiki ijayo tutaanza na undani wa kuhusu mahusiano, na kwanini ni muhimu kwenye maisha ya binadamu. Wazazi, ndugu, jamaa, marafiki, wapenzi wote wana majukumu ya kufanya kwenye maisha yako kwa muda tofauti.
Panapo majaliwa,
Fikiria kwa kina, Ishi kwa maamuzi
Watushule

