Kila Kilicho Muhimu Huja kwa Tatu
Kwanini maisha bora hujengwa kupitia mahusiano, kazi na afya.
Miezi michache iliyopita, nilifanya kazi kwenye mradi mmoja na mdogo wangu. Alitakiwa kuniletea ripoti ya sehemu aliyokuwa amefanya. Aliponitumia, ripoti yake ilikuwa imejaa makosa kwenye uandishi na herufi.
Nilimuuliza,
“Je, uliipitia kazi yako mara tatu?”
Akanijibu,
“Kwa nini mara tatu?”
Mwanzoni nilidhani anatania. Lakini nikagundua alikuwa anauliza kwa dhati kabisa.
Nikaanza kumweleza hadithi ya nilipojifunza kwa mara ya kwanza umuhimu wa kupitia kazi mara tatu.
Wakati nipo mwaka wa pili chuo kikuu cha Dar es Salaam, nilijiunga kwenye mafunzo kwenye kampuni ya KPMG Tanzania, mojawapo ya kampuni nne kubwa za ukaguzi duniani. Siku yangu ya kwanza kazini, nilipangiwa mfanyakazi mwenye uzoefu anifundishe na kuniongoza aliyeitwa Jeromini.
Alinipokea kwenye timu yake, kisha akaniambia jambo ambalo sijawahi kulisahau:
“Katika kila kazi—iwe ni ukaguzi au maisha—pitia kazi yako angalau mara tatu. Hakuna anayefanya kazi vizuri mara ya kwanza. Mara ya kwanza unapitia ili kuipanga. Mara ya pili unapitia ili kuona makosa ya wazi. Na mara ya tatu…”
Akasimama kidogo…
“…ni kuona makosa ambayo si rahisi kuyaona.”
Dada yangu alitabasamu kusikia stori ile na akaenda kuipitia kazi yake mara tatu. Aliona thamani yake mara moja.
Lakini swali lake lilibaki akilini mwangu.
Kwa nini tatu?
Nilivyozidi kufikiria, ndivyo nilivyozidi kugundua kuwa namba tatu inaonekana mara nyingi katika mambo muhimu ya maisha.
Kwa ujumla, maisha yana hatua tatu: mwanzo, katikati, na mwisho.
Viumbe hai hupitia mzunguko huo huo: kuzaliwa, kuishi, na kufa.
Hata vitu visivyo hai vinafanana: kuundwa, kuwepo, na kuharibika.
Na ukitazama kwa makini zaidi, utaona muundo huu kila mahali:
Zamani, sasa, na baadaye.
Akili, mwili, na roho.
Fikra, hatua, na matokeo.
Nidhamu, mwendelezo, na mafanikio.
Mtu, familia yake, na jamii yake.
Moja ya maeneo yanayovutia zaidi ni hisabati na uhandisi. Kuna maumbo mengi katika hisabati, lakini moja ya maumbo yenye nguvu na uthabiti zaidi ni pembetatu. Wahandisi na wajenzi hutegemea kanuni za pembetatu kwa sababu inabaki imara hata inapokabiliwa na nguvu. Ina pande tatu—na hizo ndizo zinazoipa uimara.
Hapo ndipo nilipoanza kufikiria kuhusu maisha yetu.
Sote tunatafuta nguvu na ubora
Sote tunatafuta uthabiti na uimara
Na maisha yetu yapo kati ya kuzaliwa na kufa.
Dhana hizi mbili zina kitu kimoja cha pamoja: namba tatu.
Inaonekana kwamba maisha thabiti, bora, imara na endelevu yanajengwa juu ya nguzo tatu:
Mahusiano.
Kazi.
Afya.
Nguzo hizi tatu zinaunganishwa kama pembetatu. Udhaifu katika moja yao huathiri nyingine zote. Kama maisha yako yanahisi kutokuwa sawa, kuna uwezekano mmoja wa nguzo hizi hauko sawa.
Mahusiano yanaweza kugawanywa katika familia na ndugu, mwenzi wa kimapenzi, na marafiki. Kila sehemu inaweza kujenga au kubomoa maisha ya mtu. Talaka, kuvunjika moyo, usaliti, au migogoro ya kifamilia inaweza kuathiri afya na kazi.
Kazi nayo inaweza kugawanywa katika sehemu tatu: kazi unayofanya kwa ajili ya kipato, kazi unayofanya kwa ajili ya mapenzi ya moyo, na kazi unayofanya kwa ajili ya kukua. Ni nadra kupata mtu ambaye ana vitu vyote vitatu kwa pamoja. Wengi wana kimoja au viwili. Hii ndiyo sababu watu wengi huhisi kutoridhika katika kazi zao—na hali hii huathiri pia mahusiano na afya.
Afya nayo ina vipengele vitatu: mwili, akili, na roho. Mwili unapokuwa dhaifu, kila kitu kinakuwa kigumu. Akili ikiwa si thabiti, maamuzi yanaharibika. Na roho ikipuuzwa, maisha yanaweza kuonekana hayana maana hata kama mambo mengine yanaonekana sawa.
Kwa hiyo, tumetambua vipengele vitatu muhimu vya maisha: mahusiano, kazi, na afya.
Hatua inayofuata ni kuvichunguza kwa undani zaidi, na kupata hekima ya vitendo na uzoefu utakao tusaidia kujenga maisha yenye uthabiti na mwelekeo.
Kama maisha yako hayako sawa, tafuta nini kinakosekana katika hizo tatu.
Na usikubali hitimisho hili moja kwa moja. Simama kidogo na jiulize:
Je, ni kweli?
Je, kina msaada?
Je, kinaendana?
Katika makala zijazo, tutachunguza kila kipengele kwa kina zaidi.
Fikiri kwa kina. Ishi kwa makusudi.
Watushule

