Utajiri Bora ni Ule Unaoujenga, sio Ule Unaorithi
Badala ya kusubiria urithi, tuanze kujifunza kuhusu utajiri ambao tunaweza kuujenga.
Nimekuwa nikisikia neno urithi kwa muda mrefu, lakini sikuwahi kuuelewa kwa undani mpaka pale kifo kilipogonga hodi nyumbani kwetu. Baba alipofariki, familia yetu ilipitia mchakato wa urithi.
Na hapo ndipo nilipoelewa kwa nini michakato mingi ya urithi huishia kwenye ugomvi wa familia na kesi mahakamani.
Urithi ni vitu ambavyo marehemu anaviacha kwa walio hai. Vinaweza kuwa vitu vinavyoonekana au visivyoonekana, na vinaweza kutolewa kwa familia ya karibu au hata kwa watu baki.
Kinachosikitisha ni kwamba ndugu wa karibu hutegemea urithi, wawe wamewekwa kwenye mgawanyo au la. Sisi tulipata ladha ndogo tu ya kuona pande mbalimbali zikionyesha shauku juu ya mali za baba yetu.
Siku moja nilipiga stori na ndugu yangu, nikamuuliza, hivi kuna kitu gani cha kurithi kwanza? Sikupata jibu la wazi.
Hali ya hewa ilibadilika, kana kwamba nimevunja sheria au miiko kuuliza vile. Sikukata tamaa, nikauliza tena, wewe unaujua utajiri wa baba? Sura yake ilibadilika, ghafla hofu ikamuingia, na nikagundua na yeye hana majibu kama mimi.
Siku hiyo nilijifunza kutokuchimba sana kwenye masuala ya urithi. Kwanza, watu wengi hawajui utajiri wa marehemu, hivyo wanachokiona ndicho wanachokitaka. Pili, kama mzazi wako au ndugu yako haonekani kuwa tajiri, mara nyingi hakuna kitu kikubwa cha kurithi.
Udadisi ule ulipanda mbegu ndani yangu. Niligundua kwamba mchakato mzima wa urithi unasimama juu ya utajiri. Hapo maswali yakaanza kuja.
Utajiri ni nini?
Ni nini kinachofanya familia moja iitwe tajiri na nyingine maskini?
Ni nini kinachofanya nchi moja iitwe tajiri na nyingine maskini?
Nikahamasika zaidi kutaka kujua kuhusu urithi na utajiri, na hil ndio mada kuu ya leo.
Natumaini maarifa haya yatakusaidia kuacha kutafuta utajiri na urithi kutoka kwa familia yako, na kuanza kukupa hamasa ya kujenga utajiri wako mwenyewe, na uwe na mpango bora wa nini utaacha na kwa nani, siku utakapoondoka duniani.
Kwa mujibu wa ukurasa wa Investopedia, tovuti maarufu ya masuala ya fedha na uwekezaji, utajiri ni kipimo cha thamani ya mali zote zinazomilikiwa na mtu, jamii, kampuni, au nchi.
Utajiri hupatikana kwa kuchukua thamani ya soko ya mali zote zinazoonekana na zisizoonekana, kisha kutoa madeni yote. Kwa kifupi, utajiri ni mkusanyiko wa rasilimali adimu.
Kuna maneno makuu manne yanayojenga tafsiri hii, na tutayajadili moja baada ya jingine:
Mali na madeni
Mtu, jamii, kampuni, nchi
Thamani ya soko
Rasilimali adimu
Tuanze na mali
Mali au assets ni vitu vyote vyenye thamani na vinavyoweza kutumika kuzalisha thamani zaidi. Ardhi ni mali kwa sababu ina thamani, inaweza kuuzwa, na inaweza kutumika kwenye kilimo kuzalisha mazao yanayoweza kuuzwa. Gari ni mali kwa sababu lina thamani, linaweza kuuzwa, na linaweza kutumika kusafirisha bidhaa au kutoa huduma ambazo watu wanalipia.
Pesa ni mali kwa sababu inaweza kununua mali nyingine na kuzalisha thamani zaidi. Baba alikuwa na nyumba, magari, na fedha benki alipofariki. Hizo zilikuwa sehemu ya mali zake.
Vitu kama ardhi na gari ni mali zinazoonekana. Unaweza kuziona na kuzigusa, na hizi ndizo zinazounda sehemu kubwa ya mali. Vitu kama teknolojia, hataza, na jina zuri au goodwill ni mali zisizoonekana. Hakuna anayeweza kuziona, lakini zinaweza kutumika kuzalisha thamani.
Kama una teknolojia ya kufanya jambo fulani, unaweza kuiuza kwa mtu na kuongeza thamani. Kama una jina zuri au sifa njema, unaweza kuitumia kupata vitu na kufika sehemu. Na kinyume chake pia ni kweli. Jina baya hufunga milango hata kama una uwezo.
Baba alikuwa kwenye ulimwengu wa makampuni kwa miaka ishirini na saba, hivyo jina lake la ukoo lilifahamika kwenye duru za kikazi. Sisi watoto wake tunaobeba jina lake tulirithi jina zuri lililotusaidia kwenye mazingira mbalimbali na kutufungulia milango ambayo ingekuwa migumu kufunguka bila hilo. Hiyo ni mali isiyoonekana aliyotuachia. Jina lake zuri.
Madeni au debts ni vitu vyenye thamani ambavyo mtu anaazima kutoka kwa mtu mwingine kwa makubaliano ya kuvirudisha baadaye. Baba alipokuwa anajenga nyumba yake, alichukua mkopo benki. Huo ulikuwa sehemu ya madeni yake. Pia alikuwa na gari alilopewa na ofisi kwa matumizi ya kikazi, na alitakiwa kulirudisha. Hilo nalo lilikuwa sehemu ya madeni yake.
Sasa utajiri ni kile kinachobaki baada ya kutoa madeni kwenye mali zote. Kwa upande wa baba yangu, ilimaanisha kutoa mkopo wa benki wa ujenzi wa nyumba na kuondoa gari la ofisi. Kilichobaki ndicho kilikuwa utajiri wake.
Sikuingia ndani sana kwenye kumbukumbu za baba, hivyo yawezekana alikuwa na mali au madeni zaidi ya ninayoyajua. Na hiyo ndiyo hali halisi kwa familia nyingi.
Tuangalie wamiliki wa mali
Mtu ni mtu binafsi yeyote anayetambulika kwenye nchi kwa kitambulisho chake cha taifa au hati ya kusafiria. Kama raia na mtu mzima wa nchi yoyote, una haki ya kumiliki mali. Baba yangu alifanya kazi kama mfanyakazi wa benki, alipata mshahara wake, na akafanya uwekezaji wake.
Katika maisha yake alikusanya mali kama nyumba, magari, viwanja na zaidi. Kisheria alimiliki mali zote zilizokuwa chini ya jina lake. Mtu anapofariki, kwa kawaida huacha wosia unaoeleza nani atachukua mali zake, mara nyingi mke au mume, watoto, au ndugu.
Kampuni ni shirika linalosajiliwa na mtu au kikundi cha watu ili lifanye kazi kama mtu mwingine mbele ya sheria. Kampuni inapata haki zote ambazo mtu anazo kwenye kumiliki mali, kuchukua madeni, na kulipa kodi. Vitu vingi unavyonunua au kutumia vinatolewa na makampuni. Kama unasoma makala hii kupitia simu, kuna kampuni iliyotengeneza simu hiyo, kuna kampuni ya mawasiliano iliyokuuzia laini na kifurushi cha intaneti, na kuna kampuni iliyoshona nguo unazovaa.
Jamii ni kundi la watu wenye historia au uelewa unaofanana wakifuatilia lengo la pamoja. Jamii inaweza kuwa ya kiimani, ya kijamaa, au ya kisiasa. Kisheria jamii zinaweza kumiliki mali na kuchukua madeni kwenye shughuli zao za kila siku. Kanisa au msikiti, kabila au ukoo, vyote vinaweza kuwa na mali na madeni chini ya majina yao.
Serikali ni mmiliki na mlinzi kwa niaba ya wananchi wa nchi husika. Kisheria rasilimali zote za asili zilizopo nchini ziko chini ya serikali kwa lengo la kuboresha maisha ya watu. Serikali inaweza kuchukua madeni kwa jina lake ili kutekeleza miradi itakayozalisha thamani na kukuza wananchi wake.
Tuangalie thamani ya soko na rasilimali adimu
Thamani ya soko au market value ni bei ambayo mali ingeweza kuipata sokoni. Mwanzoni tulisema mali ni sehemu ya utajiri. Sasa mali hizo zina bei ambayo watu wangekuwa tayari kulipa kama zingekuwa zinauzwa.
Nyumba ya baba ilikuwa na bei ambayo soko lilisema ndiyo thamani yake wakati ule. Alikuwa na gari aina ya Nissan X-Trail, na tungeweza kupata bei yake sokoni kama tungetaka kuliuza. Kila mali inayobaki baada ya kutoa madeni ina thamani yake ya soko.
Zamani watu walikuwa wanafanya biashara ya kubadilishana vitu kwa vitu. Siku hizi watu wanatumia pesa kama njia ya kubadilishana. Zamani, kama tungehitaji kuuza gari la baba, tungehitaji kumtafuta mtu anayehitaji gari na mwenye kitu tunachokitaka, labda chakula au nguo. Siku hizi mtu angeleta pesa taslimu, na sisi tungekabidhi gari.
Kwa kuwa pesa imekuwa njia ya kubadilishana, imejenga dhana kwamba utajiri ni pesa. Na mimi nipo hapa kukusaidia usifanye kosa hilo.
Je, umewahi kukutana na mtu mwenye pesa nyingi mfukoni lakini hana mali yoyote? Pesa ni njia ya kubadilishana inayotumika kuhamisha utajiri kutoka upande mmoja kwenda mwingine, au kutoka mali moja kwenda nyingine.
Tungeweza kuuza nyumba ya baba na kupata pesa taslimu. Hiyo ingemaanisha tumehamisha utajiri wetu kutoka kwenye nyumba kwenda kwenye pesa benki. Kisha tungeweza kuamua kutumia pesa hizo kununua viwanja vijijini kwa ajili ya kilimo. Hiyo ingemaanisha tumehamisha utajiri kutoka kwenye pesa kwenda kwenye ardhi ya kilimo.
Hivyo kazi kubwa ya pesa ni kuwa njia ya kubadilishana, lakini katika mpito pesa taslimu inakuwa sehemu ya utajiri kwa sababu ina thamani. Si kila mwenye pesa ana utajiri, lakini kila utajiri unaweza kubadilishwa kuwa pesa.
Kitu cha mwisho unachohitaji kukijua kwenye tafsiri ya utajiri ni kwamba unahusu rasilimali adimu tu. Kuna vitu vingi maishani vyenye thamani lakini si adimu, kwa mfano hewa, maji na vinginevyo.
Vitu ambavyo ni adimu, ama kwenye uzalishaji, au haviwezi kunakiliwa, au vitaisha baada ya muda, ndivyo vyenye thamani inayoviweka kwenye kundi la utajiri.
Sasa kuna vitu maishani ambavyo ni adimu na vyenye thamani lakini haviko kwenye tafsiri ya kawaida ya utajiri, kwa sababu haviwezi kuhamishwa kwa pesa. Vitu kama furaha, afya, na mahusiano vinahitajika na kila mtu, lakini hatuwezi kuviweka kwenye kundi moja na utajiri wa mtu.
Hakuna aliyetaja furaha ya baba, afya yake, au mahusiano aliyoyajenga kama vitu tunavyoweza kurithi. Lakini najua vitu hivyo vinathaminiwa sana, na wengi wetu tunaamini vitakuja baada ya kufikia tafsiri ya kwanza ya utajiri.
Kwa kuwa vitu hivi ni muhimu kwenye maisha yetu, kipindi kijacho tutazungumzia maisha mazuri, tukijikita kwenye furaha, afya, mahusiano, na kazi yenye maana.
Natumaini sasa una picha nzuri ya utajiri ni nini. Jukumu lako ni kutambua utajiri wako ulipo, kuanza kuujenga, na kuuliza maswali sahihi pale itakapofika wakati mtu anazungumzia urithi.
Panapo majaaliwa..
Uwe na furaha, Uwe na afya, Uwe huru dhidi ya mateso.
Watushule
Tunafikiri, ndipo tunakuwa.

