Usitafute mafanikio. Tafuta njia za kutokufeli.
Ni ngumu kujua kitu kitakachokupa mafanikio. Ni rahisi kutambua vitu vitakavyo kukosesha mafanikio.
Usitafute Mafanikio.
Tafuta Njia Za Kutofeli.
“Rogers, nimekusimamisha wewe pamoja na marafiki zako.”
Mwalimu mkuu msaidizi alitangaza hivi mbele ya wanafunzi wote wakati wa paredi ya Jumatatu asubuhi.
Wiki chache kabla ya siku hiyo, baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Galanos waliingia kwenye mgomo dhidi ya walimu. Walifanya madai kadhaa, na waliniomba mimi kuwasilisha malalamiko yao.
Nilikuwa waziri wa michezo mstaafu, nafanya vizuri darasani, na nikijulikana miongoni mwa wanafunzi na walimu kama “Pugu Boy.” Waliamini nilikuwa mtu sahihi wa kuwasilisha malalamiko yao. Na nilifanya hivyo.
Wanafunzi walipata wanachotaka, na maisha yaliendelea. Lakini walimu hawakusahau.
Walibeba chuki dhidi yangu na wanafunzi wachache, wakiwemo viongozi, kwa kutofanikiwa kuzuia mgomo. Wakatupa adhabu ya kusimamishwa shule kwa wale tuliokuwa kidato cha sita na wale wengine kuhamishwa.
Tulipoadhibiwa, tulikuwa miezi mitatu tu kabla ya mitihani ya taifa ya Form Six — mitihani ambayo ilikuwa njia ya kuingia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ndoto niliyoibeba kwa miaka mingi.
Adhabu yangu ilikuwa kukaa nyumbani kwa miezi mitatu yote kabla ya mitihani. Nilipaswa kuripoti shuleni usiku mmoja kabla ya mtihani, kufanya mitihani chini ya uangalizi wa polisi, na kuondoka mara moja baada ya mtihani kumalizika.
Walimu walijua kwamba hali kama hiyo, kwa kawaida, ingemsumbua mwanafunzi na kupunguza nafasi zake za kufaulu. Nilihisi vivyo hivyo niposikia habari hiyo, na marafiki zangu walilia. Ndoto zangu za masomo zilionekana kuisha.
Nilipotoka nje ya shule, moyo ulikuwa mzito, nilimpigia simu mama na kumweleza kila kitu. Alinipa pole na kusikiliza kwa undani kesi yangu. Kisha akaniuliza:
“Kwa hivyo walimu wamekuadhibu, nao wanatarajia ufeli — utafanya nini kuhakikisha hautafeli?”
Swali hilo lilibadilisha kila kitu.
Mama hakuniuliza ninachohitaji kufanya ili kufaulu. Aliuliza ninachohitaji kufanya — au kuacha kufanya — kuhakikisha sitafeli. Kuna nguvu mpya nikaipata kwenye lile swali, kwamba nikikubali kufeli walimu watakuwa wametimiza lengo.
Nilimwomba aniongeze pesa kidogo. Nikatafuta hosteli ambapo wanafunzi wengine mtaani walikuwa wanaishi na kusoma. Nikajitengenezea ratiba yangu mwenyewe — yenye masaa ya kujisomea kila siku.
Nikatafuta mitihani ya miaka iliyopita na kuitumia kutafuta maeneo yangu dhaifu. Nikasoma pamoja na wanafunzi wenzangu waliokuwa wamesimamishwa pia — tulizungumza, tulipimana, tulikataa kuruhusu adhabu ikamilishe alichotaka mwalimu.
Nilifanya hivi kwa miezi karibu mitatu. Nikarudi shule siku moja kabla ya mtihani. Miezi ikapita na matokeo yakatoka.
Matokeo yalipotolewa, nilikuwa miongoni mwa tatu bora. Nilipata A kwenye hesabu — daraja ambalo wanafunzi wachache sana walipata katika mkoa wote.
Kwa miaka kumi na tano, sikufikiria sana kuhusu stori hii ya maisha yangu. Lakini hivi karibuni, nimetambua kwamba mama yangu alinipa kitu zaidi ya moyo siku hiyo.
Alinipatia modo ya kufikiria (mental model) kwenye maisha
Modo ya Kufikiria (Mental model) ni Nini?
Modo ya kufikiria ni zana ambayo akili inatumia ili kuelewa na kutatua matatizo. Hali tofauti zinahitaji zana tofauti — kama vile daktari, mjenzi, na mwanasheria kila mmoja anabeba vyombo tofauti kufanya kazi yake. Zana ambayo mama yangu alinipatia kwenye simu hiyo ina jina.
Inaitwa inversion — yaani, kufikiria kinyume.
Kufikiria kinyume ni desturi ya kufanya kazi kwa kuangalia nyuma au kitu usichokitaka, badala ya kuwaza mbele na vitu unavyotaka.
Badala ya kuuliza nifanye nini kufaulu, unauliza ni nini kinahakikisha kufeli — kisha unaondoa mambo hayo moja baada ya jingine.
Hii Si Kukata Tamaa
Kabla sijasonga mbele, inawezekana una wazo ambalo labda linakuja akilini mwako: kufanya hivyo sio kukaribisha mawazo mabaya?
Hapana. Na tofauti hiyo ina maana.
Kukata tamaa ni hali ya kihisia. Ni kukaa na hisia ya kushindwa — kufikiria vitu vyote vibaya vitakavyotokea na kuacha kujaribu na kutenda.
Kufikiria kinyume ni zana ya kimkakati. Ni kuangalia kushindwa kama taarifa — kuiona kwa jina lake, kuelewa visababishi vyake, na kuondoa vitu hivyo.
Mtu anayekata tamaa anasema: labda nitafeli. Mtu anayetumia kufikiria kinyume anasema: hizi ndizo hali mahususi zinazozalisha kushindwa — sitaruhusu hali hizo kuwepo.
Sikukaa kwenye hosteli ile nikifikiria jinsi mitihani itakavyokwenda vibaya kwa sababu nimesimamishwa shule. Niliketi nikitambua lengo la walimu kunisimamisha shule mpaka siku ya mtihani ni ili nifeli, je vitu gani vitafanya nifeli— kisha nikaanza kuvifanyia kazi kimoja baada ya kingine.
Kuna msemo wa Kiswahili unaojulikana: haraka haraka haina baraka.
Huu, unaonekana kama ushauri wa kupunguza mwendo. Lakini ukiusoma kama kufikiria kinyume, unabeba ujumbe mkali zaidi: si kusema nenda polepole ili ufanye kazi nzuri. Unasema kukimbia kunahakikisha kupoteza unachokimbilia kukipata.
Hekima ipo katika unachokiepuka — si katika unachokiongeza. Mabibi na mababu zetu walifundisha kufikiria kinyume muda mrefu kabla haikuwa na jina.
Maswali Yanayotakiwa Kujiuliza
Kufikiria kinyume kunafanya kazi kwa sababu kushindwa kwa kawaida ni rahisi zaidi kuliko mafanikio. Kuna njia nyingi za kupata matokeo mazuri — kipaji, wakati, bahati, mitandao, juhudi, fursa. Nyingi ziko nje ya uwezo wako.
Lakini njia za kushindwa kwa kawaida ni chache, zinajirudia, na ni za uhakika. Hazikupangii. Hazitegemei mazingira. Zinaonekana kwenye kioo.
Kwa hivyo geuza swali.
Badala ya kuuliza: Nitapataje mafanikio kwenye kazi?
Uliza: Ni nini kitaharibu kazi yangu?
Badala ya kuuliza: Ninajengaje ndoa ya kudumu?
Uliza: Ni nini kinaharibu mahusiano?
Badala ya kuuliza: Ninakuwaje tajiri?
Uliza: Ni tabia zipi zinahakikisha ninabaki kuwa masikini?
Majibu ya maswali yaliyogeuzwa yanakuwa na majibu ya moja kwa moja kushinda majibu ya kuhusu mafanikio. Kwa sababu mafanikio yanaishi katika dhana tu — yako huko mbali, siku zijazo, hayaeleweki wazi.
Kushindwa, unapoangalia moja kwa moja, ni mahususi. Unaweza kuielekeza. Unaweza kuiondoa.
Sehemu Sahihi Ya Kutumia Mental Model Hii
Katika kazi yako:
Fikiria miaka mitano ijayo ya maisha yako ya kikazi.
Jiulize ni nini kitaharibu mwenendo wako wa kazi.
Majibu ya kawaida ni pamoja na: usimamizi mbaya wa fedha, kuharihu mahusiano muhimu, kukaa katika nafasi ambazo hauwezi kukua, uongo, uvivu na vingine kadhaa.
Ni vitu vingapi kati ya hivyo tayari vipo kwenye maishani mwako?
Katika mahusiano yako:
Kuna mambo zaidi ya maelfu ambayo watu husema yatafanya uhusiano udumu — mawasiliano, kujitolea, wakati wa pamoja, maadili yanayofanana. Yote hayo ni kweli.
Lakini kuna idadi ndogo sana ya mambo yanayoharibu uhusiano kwa uhakika: dharau, uongo, kupuuza kunakokuwa kawaida, malalamiko yasiyo fanyiwa kazi, usaliti na mawasiliano mabovu.
Jiulize mambo yapi kati ya hayo yapo kwenye mahusiano yako sasa hivi?
Katika fedha zako:
Watu wengi wakifikiria pesa wanawaza namna ya kuzipata na kuwa matajiri.
Kufikiria kinyume kunauliza swali tofauti: ni mifumo gani ya matumizi inayohakikisha hautaweza kuwa na utajiri — bila kujali kipato chako?
Jibu kwa kawaida si gumu. Ni mfumuko wa maisha unaosogea sambamba na ongezeko la mshahara. Ni kutokuwepo kwa utaratibu wowote wa akiba ya moja kwa moja. Ni kuchukulia mkopo kama mapato ya ziada. Kuishi maisha ya starehe ambayo hauna uwezo nao. Kuwa na chanzo cha mapato kimoja na ambacho kinaweza kukatishwa muda wowote.
Jiulize vitu vipi tayari vipo kwenye maisha yako sasa hivi kwenye maswala ya fedha?
Swali Linalostaahili Kuwa Kichwani Kila Siku
Fikiria eneo moja muhimu la maisha yako sasa hivi — kazi yako, fedha zako, mahusiano, afya yako. Adha kujiuliza ni namna gani utafanikiwa.
Sasa uliza kinyume:
Ni nini kitasababisha unashindwa kufanikiwa?
Andika majibu ya ukweli na uhalisia wa maisha yako. Usijidanganye.
Kisha angalia orodha hiyo na ujiulize: Ni mangapi kati ya haya tayari ninayafanya?
Orodha ya majibu yako ndio orodha ya vitu vinavyoweza kubadili maisha yako.
Panapo majaliwa
Fikiria kwa kina. Ishi kwa makusudi.
Watushule

