Pesa Inazaa Pesa. Na Pesa Inayozaa Pesa Huzaa Pesa Zaidi
Tafakari kuhusu kukua — katika pesa, watu, na ujuzi.
Wiki iliyopita nilirudi Dar es Salaam. Nilipita Posta.
Unajua ile sehemu ya mji yenye mnara wa Askari umesimama katikati. Magari yanazunguka. Watu wanapita haraka haraka. Daladala. Harufu ya mahindi ya kuchoma pembeni. Mnara umesimama tuli, na mji unaendelea kutembea.
Nimepita Mnara wa Askari mara nyingi sana. Wiki iliyopita ilikuwa tofauti. Nilipojikuta naingia kwenye barabara ndogo ya dharura nikasimama. Sikuwa nimepanga kusimama. Nilisimama tu.
Niliangalia upande wa pili wa barabara, mahali ambapo zamani ilikuwa Tanzania Posta Bank. Jengo hilo sasa ni kitu kingine. Walihama. Wana jina jipya. Tanzania Commercial Bank.
Nilipokuwa nimesimama pale, niliikumbuka ile benki ya zamani. Ile niliyoingia kwa mara ya kwanza. Baba alikuwa ameniagiza kumwona meneja wa tawi. Meneja huyo alipaswa kunisaidia kufungua akaunti yangu ya kwanza.
Nilikuwa na miaka kumi na nne. Pengine kumi na tano.
Baba alikuwa amenisukuma kwa wiki nyingi. Fungua akaunti. Fungua akaunti. Sikutaka. Sikuwa na pesa. Ningeweka nini ndani? Lakini alishikilia. Jinsi wazazi wanavyoshikilia mambo usiyoyaelewa.
Basi nikaenda. Nikajitambulisha. Nikamuulizia meneja wa tawi.
Ofisi yake ilikuwa kwenye kona kabisa. Dirisha la ofisi yake lilikuwa likitazama moja kwa moja Mnara wa Askari. Niliketi kwenye kiti cha mbao. Yeye aliketi kwenye kiti cha ngozi.
Tulipiga story kidogo. Akamwambia msaidizi wake aanze kunifanyia utaratibu wa kufungua akaunti. Msaidizi wake alijaza fomu. Nikatia sahihi. Sahihi ni mbaya. Nisingesaini hivyo leo. Walinipa kadi na kitabu kidogo cha hundi.
Lengo likatimia. Nikapata akaunti yangu ya kwanza.
Kwa miaka michache, niliitumia ile akaunti. Pesa za matumizi. Pesa za likizo. Chochote kilichopita mikononi mwangu wakati wa sekondari kilienda kwenye akaunti hiyo. Kisha sekondari nikamaliza. Nikaendelea na maisha.
Nikasahau.
Nilisahau kabisa kuhusu ile akaunti. Kadi ya benki nilisahau kwenye madroo. Kitabu cha hundi kilikuwa kwenye mafaili. Akaunti ikaacha kupokea miamala.
Kwa miaka.
• • •
Wiki iliyopita, nilipokuwa nimesimama pale karibu na Mnara wa Askari, nikiangalia mahali ambapo benki ilikuwa — yote yakanijia kichwani.
Nilirudi nyumbani jioni hiyo. Nilianza kutafuta. Nilifungua faili ambazo sikuzifungua kwa miaka. Bahasha za zamani. Karatasi za zamani. Nikaipata. Kadi. Namba ya akaunti. Hata taarifa ya mwisho ya akaunti.
Taarifa ilisema: shilingi 90,000.
Tisini elfu. Ndio salio nililoacha siku niliyoacha kutumia akaunti.
Niliketi na karatasi. Nikafikiri — Je akaunti bado ipo hai? Pesa bado iko? Imekuwaje sasa?
Asubuhi iliyofuata nilienda benki. Benki mpya. Jina jipya. Jengo jipya. Wahudumu ambao hawakuwa wameajiriwa nilipofungua akaunti.
Niliwapa taarifa zangu. Wakaangalia. Wakatafuta. Wakaangalia tena.
“Samahani. Akaunti hiyo ilifungwa miaka mingi iliyopita. Unaweza kufungua nyingine kama unataka.”
Nikasema asante, sihitaji. Nikageuka na kuanza kuondoka.
Kisha nikasimama. Nikamgeukia na kumuuliza;
“Salio langu la mwisho lilikuwa shilingi 90,000. Mwaka 2008. Ingekuwa kiasi gani sasa kama akaunti ingekuwa haijafungwa?”
Hakusema chochote. Akaenda kwenye kompyuta yake. Akabonyeza bonyeza keyboard. Akaniangalia. Akatabasamu. Akachukua karatasi. Akaandika kitu. Akaikunja. Akaiingiza kwenye bahasha yenye nembo mpya. Akanikabidhi.
“Fungua ukifika nyumbani.” Akasema.
Nilipenda drama aliyongezea ya kuficha, ikaniongezea hamasa ya kutaka kujua. Niliweka bahasha kwenye begi. Nikaondoka.
• • •
Kiasi cha awali: shilingi 90,000, mwaka 2008
Riba: 13% kwa mwaka
Riba juu ya riba kila mwaka
Shilingi 562,500
Hisia zilikuja nyingi sana kwa wakati mmoja. Pesa yangu ilikuwa imekua kutoka shilingi 90,000 hadi 562,500. Sikufanya chochote.
• • •
Haikuwa uchawi kilichotokea, Ni kitu kina maelezo rahisi sana.
Compounding. Kwa Kiswahili — riba juu ya riba.
Ni neno la kwenye ulimwengu wa fedha.
Pesa ukiweka benki hupata riba.
Riba ukiiacha benki nayo hupata riba.
Kisha riba hiyo hupata riba. Kidogo mwanzoni. Kisha unaanza kuona ikikua. Kisha inakuwa ya kushangaza kadri muda unavyoenda.
Inasemekana Albert Einstein, mwana sayansi maarufu sana aliiita riba juu ya riba kuwa maajabu ya nane ya dunia. Iwe alisema au la, yeyote aliyeshuhudia ufanyaji kazi wa riba juu ya riba anajua.
Pesa ikiwekezwa inazaa pesa.
Pesa inayozaa pesa, huzaa pesa zaidi.
Lakini si hicho tu ninachotaka tutafakari leo hapa Watushule.
Compounding au riba juu ya riba si dhana ya fedha tu. Ni dhana ya maisha.
• • •
Compounding katika mahusiano
Fikiria watu walio muhimu katika maisha yako. Wale wanaopokea simu zako. Wale wanaokupigia wakipata habari njema, na wale wanaokupigia wakipata habari mbaya.
Mlikutana lini?
Kwa wengi wetu, zamani sana. Sekondari. Chuo. Kazi ya kwanza. Biashara ndogo uliyojaribu kabla ya hii. Kikundi cha kanisa au msikiti. Mtaa.
Hukupanga wawe muhimu. Ilijitokeza tu. Ulipiga simu hata wakati hauhitaji chochote. Ulisaidia hata kama ilikugharimu kidogo. Ulikumbuka siku za kuzaliwa. Ulihudhuria misiba. Ulituma “nimekukumbuka” bila sababu yoyote.
Mwaka hadi mwaka, mahusiano yalikuwa yanakua. Hukuyaona.
Rafiki wa Form Three anakuwa mtu wa kukuajiri miaka kumi na tano baadaye. Binamu uliyemsaidia kazi za shule anakuwa mtu wa kukuunganisha na mteja. Jirani aliyekula nawe ulipokuwa hauna kitu anakuwa mlezi wa mtoto wako.
Mahusiano usiyoyachunguza mara kwa mara ndiyo yanayoota mizizi ya kina.
Mafanikio kwenye maisha yanaletwa na mahusiano yaliyojengwa kwa miaka mingi sana kwa wazo la riba juu ya riba. Unaishi na mtu vizuri na yeye anaishi vizuri na wewe. Na huyo mtu atakutambulisha kwa mtu mwingine vizuri na yeye ataishi na wewe vizuri.
Na mahusiano ya muda mrefu ndio huleta ukaribu, upendo, msaada na jamii ya watu bora kwenye maisha yako. Miaka itapita kama ile akaunti yangu ya benki. Lakini kuna siku mahusiano hayo ya muda mrefu yatakuja kufanya makubwa zaidi kwenye maisha yako bila kutegemea.
• • •
Compounding katika ujuzi
Ujuzi nao unakua.
Ukiwa na miaka kumi na tisa, unajifunza kuandika vitu. Haionekani kama jambo kubwa. Ukiwa na miaka ishirini na mbili, unajifunza kusikiliza kwenye mkutano kabla ya kuongea. Haionekani kama jambo kubwa. Ukiwa na miaka ishirini na tano, unajifunza kujielezea. Hiyo nayo inaonekana ndogo.
Viweke pamoja. Miaka ishirini ya ujuzi mdogo mdogo, umepangwa juu ya mwingine. Jinsi unavyofikiri. Jinsi unavyojielezea na kuwasiliana na watu. Jinsi unavyoshughulika na watu wagumu. Jinsi unavyojadiliana. Jinsi unavyoandika. Jinsi unavyojishikilia mambo yanapoharibika.
Mlundikano huo ndio watu wanaomaanisha wakisema “uzoefu.” Si muda. Muda peke yake hautoi chochote. Ni ujuzi mdogo. Uliojirundika kwa miaka mingi.
Ukweli mchungu — watu walioanza wakiwa na miaka kumi na nane ni vigumu kuwafikia ukiwa na miaka thelathini na tano. Si kwa sababu wana akili zaidi. Wana miaka mingi zaidi “ya ujuzi juu ya ujuzi.”
Mtu aliyeanza biashara miaka mitano nyuma ana ujuzi juu ya ujuzi ambao ni bora kushinda anayeanza biashara leo. Kwenye maisha yako tafuta mbinu ya kujenga ujuzi juu ya ujuzi. Miaka mingi ikipita wewe utakuwa bora kwa sababu akaunti yako ya ujuzi itakuwa imekua.
• • •
Uhalisia
Pesa. Mahusiano. Ujuzi. Vyote vinakua. Lakini kwa sharti moja tu.
Lazima uviache muda wa kutosha.
Unapanda mbegu. Huichimbui kila wiki kukagua. Hapo ndipo sehemu ngumu. Kizazi chetu kinataka risiti leo. Tunapost na kuangalia likes ndani ya dakika tano. Tunatuma ujumbe na kungoja blue ticks. Tunaanzisha biashara halafu tunauliza kwa nini hatujatajirika mwezi wa tatu.
Compounding haifanyi kazi hivyo.
Compounding inakuomba uuamini muda. Kufanya jambo dogo leo. Na kesho. Na kesho kutwa. Na uache kuhesabu.
Vitu vinavyokua zaidi maishani mwako ni vile unavyoacha kuvikagua.
Kutoka shilingi 90,000 — katika akaunti nisiyoitoa, nisiyoiongezea, nisiyoikumbuka — pesa zilikua. Zaidi ya mara sita ya kile nilichoacha pale.
Niliondoka benki nikifikiri vitu vingi sana.
Nilifikiria ingekuwaje kama ningekuwa nikiongeza akiba. Fikiria kama kila mwezi ningekuwa nikiilisha kiasi kidogo. Fikiria kama ningefanya hivyo katika mahusiano. Katika ujuzi.
Chochote ulicho leo. Umri wowote. Hatua yoyote. Kuna akaunti mahali katika maisha yako unayoweza kuifungua leo. Ujuzi. Uhusiano. Tabia. Kiasi kidogo cha kuhifadhi kila mwezi kwenye jambo lenye maana.
Ifungue sasa. Isahau kwa muda. Acha muda ufanye kazi usiyoweza kufanya wewe.
• • •
Baba alinisukuma kufungua akaunti hiyo nilipokuwa sielewi kwa nini.
Alikuwa mtaalamu wa fedha. Alikuwa anafanya kazi benki. Alikuwa mtu aliyeelewa, kama wazee wanavyoelewa, kwamba unapanda vitu kabla hujavihitaji. Na vitu hivyo huongezeka
Jenga mahusiano yanayokua.
Jenga ujuzi unaokua.
Jenga pesa inayokua.
• • •
Hii ni Watushule.
Tunafikiri. Hivyo tunakuwa.
Hadi wiki ijayo — kwaherini.

