Ndoto huanzisha safari; mifumo huikamilisha.
Acha kutengeneza malengo tu, anza kuunda mifumo kwenye maisha yako
Umewahi kuitazama filamu The Terminator iliyoigizwa na Arnold Schwarzenegger?
Filamu hiyo inamtambulisha Arnold kama Terminator, roboti muuaji asiyekata tamaa. Katika simulizi ya filamu hiyo, binadamu wako vitani dhidi ya mashine zinazoongozwa na akili bandia inayoitwa Skynet. Terminator ana misheni, na yuko tayari kufanya chochote ili kuitimiza.
Arnold Schwarzenegger alikuwa na mistari isiyozidi ishirini katika filamu nzima. Lakini mstari mmoja ukawa wa kihistoria: “I will be back.” Alikuwa na mwonekano wa kipekee. Alivaa koti jeusi la ngozi na miwani ya jua usiku. Mwendo wake ulikuwa wa taratibu, wa makusudi, na wenye harakati za kiroboti.
Sote tulitaka kuwa kama yeye.
Wakati huo hatukuwa na njia ya kuwajua waigizaji zaidi ya kile tulichokiona kwenye filamu.
Miaka ikapita, na intaneti ikaanza kupatikana kwenye internet café nyingi. Moja ya vitu vya kwanza nilivyotafuta mtandaoni ilikuwa Arnold Schwarzenegger. Niligundua kitu kimoja: Arnold aliigiza nafasi ya Terminator vizuri sana kwa sababu kwa namna fulani, ilifanana na maisha yake mwenyewe.
Terminator alikuwa na misheni ya kutekeleza, na alifanya kila kilichohitajika ili kufanikiwa. Katika maisha halisi, Arnold alifuata njia inayofanana na hiyo kwa kujiwekea malengo ya wazi na kufanya kazi bila kuchoka kuyafikia.
Alikuwa kijana mwenye ndoto kubwa huko Austria. Alijiunga na jeshi. Siku moja, alimwona Reg Park kwenye televisheni akishinda mashindano ya kujenga mwili au body building. Akavutiwa na kutamani kuwa kama yeye.
Akajiwekea lengo la kuwa body builder (mjenga mwili) kama shujaa wake, kisha kuondoka Austria, kwenda Hollywood, na kuwa mwigizaji.
Filamu The Terminator ilitoka tarehe 26 Oktoba 1984, miaka saba kabla sijazaliwa.
Niliitazama filamu hiyo miaka kumi na nane baadaye. Nililipa shilingi hamsini za Kitanzania kuingia kwenye chumba chenye giza. Walikuwa wamekificha na kukifunika kwa mapazia na mazulia. Viti vilivyovunjika na mabenchi yaliyokuwa yakianguka vilizunguka televisheni ndogo ya Chogo.
Wakati mimi natazama filamu ya Terminator ilimaanisha kuwa ndoto ya Arnold ilikuwa imetimia. Kwangu, hiyo ilikuwa tafakari ya kuvutia sana. Kuvutiwa na mtu, kutengeneza lengo, na kulifikia. Ilionekana kama njia bora ya kuishi maisha.
Zaidi ya miaka kumi na nane imepita tangu nilipotimiza lengo langu la kwanza kubwa maishani. Nililiandika kwenye notebook na kulisoma kwa umakini mkubwa, nikiwa nimevutiwa na Arnold Schwarzenegger. Nilipokuwa kids to cha nne Shule ya Sekondari Pugu, nilitengeneza lengo langu la kwanza na kuliandika: “kusoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.”
Niliweka lengo hilo kwa sababu binamu yangu alikuwa amesoma katika chuo hicho miaka michache kabla. Kama Arnold, nilikuwa na lengo langu la kwanza.
Nilipata sababu zaidi za kusoma kwa bidii. Nilisisimka kutafuta namna ya kuingia katika chuo kikuu cha Dar es salaam. Nilijikita kwenye vigezo vya udahili, kozi sahihi, na mambo mengine. Kila nilipopata muda wa ziada, nilipanda basi kwenda chuoni. Nilipenda kuwaona wanafunzi waliokuwa wamefanikiwa na waliobahatika kusoma pale.
Miaka mitatu baadaye, nilikuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, nikisoma Shahada ya Biashara katika Fedha. Nilikuwa nimetimiza lengo langu la kwanza. Nikakumbuka lengo la kwanza la Arnold, kushinda taji la Mr. Universe.
Wakati huo, hilo lilikuwa moja ya mashindano maarufu zaidi ya kujenga mwili duniani. Lilikuwa ni taji lilelile ambalo shujaa wake, Reg Park, alikuwa amewahi kushinda.
Baadaye nilitengeneza malengo mengine machache chuoni ili kuthibitisha kama mbinu hiyo kweli inafanya kazi. Nilisema nilitaka kuwa na gari langu mwenyewe kabla ya kuhitimu, nikiwa mwaka wa tatu. Nilitaka kupata kazi mara tu baada ya kuhitimu. Pia nilikuwa na lengo la kuanzisha kampuni yangu ya kwanza kabla ya kuhitimu.
Wiki moja kabla ya siku ya mahafali yangu, nilikuwa na gari langu la kwanza, Toyota Celica nyekundu, lililoagizwa kutoka Japan. Nilikuwa na mkataba wa kazi na moja ya kampuni kubwa nne za ukaguzi wa hesabu, PwC, na nilikuwa na kampuni yangu, au niseme startup.
Kwangu, hilo lilimaanisha kuwa kuweka malengo kuna faida kubwa kwenye maisha. Arnold alishinda mataji matano ya Mr. Universe na mataji saba ya Mr. Olympia katika safari yake ya kujenga mwili. Aliigiza kwenye zaidi ya filamu arobaini za Hollywood. Hata akawa Gavana wa California.
Nilisisimka sana kuwaambia watu umuhimu wa kuwa na malengo maishani. Lakini baadaye nikagundua kuwa watu wengi huja na malengo na kuhamasika. Baada ya miezi michache, hupoteza hamasa na kuacha.
Nimeona hilo kwa ndugu zangu, marafiki, jamaa, na hata watu nisiowajua. Ilinifanya niwe na udadisi wa kujua kwa nini malengo hufanya kazi kwa baadhi ya watu, lakini hayafanyi kazi kwa wengine. Nilijiuliza ni nini kilinifanya nifanye kazi kwa bidii zaidi nilipokuwa na malengo kuliko wakati ambao sikuwa nayo.
Udadisi huo ulinifanya nichunguze zaidi kuhusu malengo, ndipo nikakutana na dhana ya mifumo. Arnold hakuishia tu kuweka malengo au kuwa na ndoto. Alichotengeneza hakikuwa malengo pekee.
Ndoto na malengo peke yake hayana maana. Unahitaji mfumo.
Arnold alianza na ndoto, kisha akaivunja kuwa malengo, na hatimaye akatengeneza mfumo. Ili kushinda Mr. Universe, alipaswa kufanya mazoezi mara tatu kwa siku, kula sana, na kujifunza kila alichoweza kuhusu mashindano hayo.
Alipaswa kujitokeza hata alipokuwa amechoka, mgonjwa, hana hamasa, au amechelewa. Jeshi lilitishia kumfukuza, lakini bado alipaswa kuwepo.
Ili kupata kazi kabla ya kuhitimu, nilihitaji kujifunza kuhusu waajiri wakubwa. Nilipitia usaili wao wa nyuma na kufanya mazoezi ya aptitude tests. Pia nilihudhuria kila career day niliyoweza kuipata.
Nilikosa baadhi ya vipindi na quiz. Pia nilipoteza muda ambao ningeutumia kutazama filamu, kukaa na marafiki, na kucheza mechi za mpira nilizotamani sana kucheza.
Nilianza kwa sababu ya ndoto na lengo. Niliendelea kwa sababu ya mfumo nilioujenga.
Hii ndiyo njia bora.
Msingi bora wa mfumo wowote bado ni ndoto na lengo. Unaweza kuota chochote, lakini hakitakuwa na maana mpaka ukibadilishe kuwa lengo. Hii ndiyo njia ya vitendo zaidi niliyoiona katika kutengeneza malengo, nilijifunza kutoka kwa marehemu Jim Rohn.
Kwanza, orodhesha matamanio yako yote, fikra zako zote, na ndoto zako zote.
Chagua matamanio, fikra, na ndoto hamsini ambazo ungependa kuzifuata kama ungepata nafasi.
Punguza orodha hiyo hadi kubaki na zile kumi na sita ambazo unaweza kuanza ndani ya miaka mitano ijayo.
Gawa malengo hayo kumi na sita katika makundi manne. Kuwa na matamanio au ndoto nne ambazo zinaweza kuchukua miaka mitano kutimia. Kuwa na matamanio, ndoto, au fikra nne ambazo zinaweza kuchukua miaka mitatu. Kuwa na malengo manne ambayo yanaweza kuchukua mwaka mmoja. Kisha kuwa na malengo manne ya mwisho ambayo yanaweza kuchukua wiki chache au miezi michache.
Kisha ndipo inapokuja sehemu muhimu zaidi. Kwa kila moja ya malengo hayo kumi na sita, jaribu kujibu maswali haya:
Kwa nini unataka kutimiza tamanio, ndoto, au fikra hiyo?
Kwa nini usijaribu kuitimiza na uone maisha yatakupeleka wapi?
Kwa nini usiwe wewe wa kujaribu kuitimiza?
Kwa nini usianze sasa hivi?
Ukishayapanga malengo yako kumi na sita ndani ya miaka mitano, upande wa vitendo wa maisha unaanza. Unahitaji kutengeneza mfumo unaozunguka malengo yako.
Unahitaji kujenga tabia za kila siku na mazingira ambayo tabia hizo zinaweza kustawi. Dumisha mfumo huo kwa muda wote unaohitajika mpaka utimize matamanio, malengo, au ndoto zako.
Tabia hizi ndizo shughuli za kila siku zitakazokupeleka kwenye kufikia malengo hayo.
Ili kushinda mashindano ya kujenga mwili, kwanza Arnold alipaswa kuishi kama mjenga mwili. Alipaswa kufanya mazoezi kila siku, kula vizuri, kujifunza mchezo huo, na kupumzika.
Alijitosa kwenye kujenga mwili kwa kusoma kila jarida aliloweza kupata na kutazama vipindi vya televisheni vilivyohusiana na mchezo huo. Pia alijitoa kwenye ratiba kali ya mazoezi, akifanya mazoezi kama mtaalamu mara mbili au tatu kwa siku.
Alifanya hivyo mpaka akashinda mashindano.
Mara baada ya kuamua kile alichotaka kutimiza, alijikita kwenye mfumo wa kila siku aliopaswa kuufuata. Siku nyingine hakuwa na hamasa, lakini alipaswa kufanya mazoezi kwa sababu mfumo ulimtaka afanye hivyo.
Siku nyingine alikuwa na shughuli nyingi, lakini mfumo ulimsukuma kutafuta muda wa kusoma na kujifunza kuhusu kujenga mwili. Siku nyingine alihisi kukata tamaa kwa kuhofia kuwa huenda asifanikiwe, lakini mfumo wake ulimsukuma kufanya mazoezi na kupumzika.
Na alifanya hivyo pia kwenye uigizaji Hollywood. Alitengeneza mfumo ambao ungemsaidia kuwa mwigizaji tunayemjua leo. Alipaswa kujifunza kuigiza, kusoma kuhusu lafudhi, na kuandaa mwili wake kwa nafasi za uigizaji.
Nilipotengeneza ndoto, lengo, au fikra ya kuwa na gari kabla ya kuhitimu, sikuwa na kazi wala biashara. Nilipaswa kuchagua gari la ndoto, kujua bei yake, na kutafuta njia za kuweka akiba, kuomba, kubembeleza, kupata kipato, au kukopa ili kulipata.
Nilianza baadhi ya biashara ambazo zingenipa faida ya ziada kunisaidia kununua gari, lakini biashara hizo zilifeli. Niliomba msaada kwa watu wengi; wengine walinisaidia, wengine walinikataa.
Nilijaribu kuweka akiba kutoka kwenye pesa ya matumizi ya chuo, wakati mwingine ilifanikiwa na wakati mwingine haikufanikiwa. Nilikopa kwa marafiki na watu wengine; wengine walinipa, wengine walikataa.
Lakini kabla ya kuhitimu, nilikuwa na gari.
Nilihudhuria zaidi ya usaili ishirini ndani ya miezi miwili nikiwa chuoni. Wakati mwingine usaili ulikuwa katikati ya mitihani. Hilo lilitokana na kipindi kirefu cha kutuma CV; baadhi ya waajiri walikataa maombi yangu, wengine waliniita kwenye usaili.
Nilisoma vitabu na makala nyingi kuhusu usaili; nyingine nilizielewa na nyingine sikuzielewa. Nilipiga simu kwa watu wengi kuomba taarifa za ndani, msaada, na connection kwenye sehemu za kazi. Wengine walipokea simu zangu, wengine walikata simu, na wengine hata waliniblock.
Sikuacha kwa sababu nilikuwa na mfumo wa kufuata baada ya kujitoa kwenye malengo hayo. Kila siku, mfumo wangu ulinisukuma kufanya mambo kadhaa. Nilisoma kuhusu kazi na usaili. Nilituma CV yangu kwa mtu. Niliwakumbusha wengine kuhusu CV niliyotuma. Pia nilifanya mazoezi ya maswali ya usaili kwa usaili wowote uliokuwa mbele yangu.
Nilipokuwa na lengo la kujenga misuli na kuwa na six-pack, nilitengeneza mfumo. Kila siku baada ya vipindi vya chuo, nilienda gym ya chuo, nilifanya stretching, nilifanya mazoezi ya makundi mawili ya misuli, kisha nikacheza mpira.
Nilihakikisha kila siku nakula protini nyingi, hasa mayai, ndizi, na kuku. Nilihakikisha nakunywa maji mengi na kupumzika vya kutosha. Pia nilikuwa naenda YouTube mara kwa mara kutazama video nyingi kadiri nilivyoweza kuhusu kunyanyua vyuma.
Pia nilimuuliza maswali mengi Teacher Swai, kocha rasmi wa chuo. Naye alikuwa na misuli mingi. Pia nilishauriana na wanafunzi wengine kadhaa waliokuwa na uzoefu wa kunyanyua vyuma.
Na mfumo huo ulinitaka nifanye hivyo mpaka nitimize lengo. Nilipaswa kufanya hivyo baada ya vipindi na mitihani. Nilipaswa kufanya hivyo nilipokuwa nimechoka. Nilipaswa kufanya hivyo hata nilipokuwa sina pesa nyingi za kununua kuku na mayai. Nilipaswa kufanya hivyo hata Teacher Swai alipokuwa hayupo. Ulikuwa mfumo niliopaswa kuufuata.
Kila nilipogundua kuwa sifuati mifumo yangu, nilitambua kuwa sitatimiza ndoto yangu. Na hilo lilinikumbusha kwa nini niliitaka ndoto hiyo tangu mwanzo. Sababu yangu ilipokuwa imara, nilijikuta nikirudi kwenye mfumo wangu mara moja.
Nilijifunza kuwa wakati mwingine maisha yanaharibu utaratibu na mifumo, na unaweza kuacha mfumo wako kwa siku moja au mbili. Lakini nilikuwa na uwezekano mkubwa wa kufanikiwa nilipojisukuma nisiache zaidi ya siku tatu zipite bila kufuata mfumo wangu.
Nimekuwa nikitumia mfumo huo huo kwa zaidi ya miaka kumi na nane sasa, na nitaendelea kuutumia milele. Nimeuona kuwa wa vitendo na unaofaa kwa kufanikisha lengo lolote.
Hiki ndicho unachopaswa kufanya ili kutimiza ndoto, matamanio, au mahitaji yako;
Orodhesha matamanio yako yote, fikra zako zote, na ndoto zote unazotaka zitimie ukiwa hai, au hata baada ya wewe kufariki.
Chagua zile bora hamsini za kuanzia.
Kutoka kwenye hizo hamsini, chagua kumi na sita muhimu zaidi kwako kwa sasa.
Gawa malengo hayo kumi na sita kulingana na muda unaokadiria kuyatimiza, kuanzia wiki chache mpaka miaka mitano.
Inashauriwa uwe na malengo manne unayoweza kutimiza ndani ya wiki chache au miezi michache.
Chagua mengine manne kwa malengo ya mwaka mmoja, kisha mengine manne kwa kipindi cha miaka mitatu. Malengo manne ya mwisho yawe yale unayolenga kuyatimiza ndani ya miaka mitano.
Kwa kila tamanio, fikra, au ndoto, chukua muda kujiuliza maswali haya:
Kwa nini unataka kutimiza tamanio, ndoto, au fikra hiyo?
Kwa nini usijaribu kuitimiza na uone maisha yatakupeleka wapi?
Kwa nini usiwe wewe wa kujaribu kuitimiza?
Kwa nini usijaribu sasa hivi?
Ukisharidhika na hilo, ndipo tengeneza mfumo kwa kila lengo.
Tengeneza tabia na orodha za mambo ya kufanya kila siku au kila wiki mpaka ufikie malengo yako.
Jisukume kila wakati kufuata mfumo huo, bila kujali nguvu ulizonazo, hamasa, matatizo, au vikwazo. Pale changamoto zinapotokea na ukaruka siku moja au mbili, jiambie kuwa utarudi kwenye mfumo haraka iwezekanavyo.
Kanuni bora ni kuahidi kutoruhusu zaidi ya siku tatu zipite bila kufuata mfumo wako.
Katika kufuatilia lengo langu la uandishi, nimejiahidi kutoruhusu zaidi ya siku tatu zipite bila kuandika kitu cha nilichojifunza. Nimejiahidi pia kutoruhusu zaidi ya siku tatu zipite bila kufanya mazoezi, hata kama itamaanisha kutembea au kufanya stretching.
Kuwa mwangalifu usiwe na tamaa kupita kiasi unapotengeneza mfumo wako. Ni rahisi sana kubebwa na hamasa. Unaweza kufanya vitu kwa kasi zaidi, kwa ukubwa zaidi, au kwa nguvu zaidi, lakini visiwe endelevu.
Watu wengi hutengeneza lengo au kuwa na ndoto ya kuwa fiti, mara nyingi watu wenye uzito mkubwa wanaotaka kupunguza uzito. Wananunua vifaa vipya vya mazoezi, wanalipia gym, na kusema, “New Year, New Me.” Yani mwaka mpya na mambo mapya. Lakini kufikia katikati ya Januari, wengi hurudi kwenye tabia zao za zamani.
Watu hawa walitengeneza mfumo uliowazidi nguvu na ambao haukuwa endelevu. Ni rahisi kuanza kwa kutembea mara tatu kwa wiki, kisha taratibu kuhamia kwenye kutembea kila siku. Kutoka hapo, unaweza kuongeza kasi au umbali kabla ya kuongeza kukimbia au mazoezi ya gym.
Na ukiwa na hamasa, nenda gym. Ukiwa na shughuli nyingi, tembea. Lakini kwa ujumla, bado unaendelea kufuata mfumo.
Ni sawa kuwa na ndoto na malengo, lakini maisha hutokea pale unapofuata mfumo wako kwa uthabiti.
Mpaka wakati mwingine,
Fikiri kwa Kina. Ishi kwa Makusudi.
Watushule

