Maisha Mazuri ni Yapi?
Afya njema. Familia yenye utulivu. Utajiri endelevu. Mtu wa kumpenda. Na jambo lenye maana la kufanya.
Nimelelewa na mama peke yake. Alipambana kuwahudumia watoto wake watano, sikuona kama yale yalikuwa ni maisha bora. Kwa hiyo, niliamini kuwa kuwa na wazazi wote wawili ndiyo ilikuwa maana ya maisha mazuri.
Niliwaonea wivu marafiki zangu na hata watu nisiowajua waliokuwa na wazazi wote wawili nyumbani. Nilitazama familia zao zikifanya mambo kwa pamoja na kujiuliza maisha kama yale yalikuwaje.
Lakini baadaye nilipata nafasi ya kuwa karibu na baadhi ya familia hizo. Nikagundua kwamba kuwa na wazazi wote wawili hakukumaanisha kila mara kuwa familia ilikuwa na furaha.
Maisha mazuri yalikuwa na maana kubwa zaidi ya nilivyofikiri.
Nilisoma katika shule za sekondari za serikali. Madarasa yalikuwa yamejaa wanafunzi. Walimu hawakutosha, na miundombinu ilikuwa mibovu. Niliamini kwamba maisha yangekuwa rahisi zaidi nitakapofika chuo kikuu.
Kisha nikafika katika moja ya vyuo vikuu bora nchini Tanzania, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Nikapangiwa kuishi katika chumba cha hostel kilichokuwa na wanafunzi mara mbili zaidi ya uwezo wake. Wahadhiri wachache walikuwa bora sana. Kuna wengi walikuwa wa kawaida, na wengine walikuwa chini ya kiwango.
Nilipokuwa chuo kikuu, niliamini kuwa kuhitimu na kupata kazi nzuri kungenipa maisha mazuri. Niliwaza kuhusu kupokea mshahara kila mwezi na kupandishwa cheo kila mwaka.
Kisha nikapata kazi kabla hata sijahitimu chuo kikuu.
Nilikaribishwa na kazi za usiku, kuamka mapema, barua pepe za mwishoni mwa wiki na mabosi wabinafsi walioleta chuki zao binafsi kazini. Promosheni zilichelewa na mshahara ulikuwa hautoshi kumbe. Sikuweza kuona maisha mazuri bado.
Baada ya hapo, niliamini kuwa kujiajiri ndiyo ilikuwa njia ya kupata maisha mazuri. Unaamka muda unaotaka, unafanya kazi na watu unaowachagua na unaendesha mambo kwa namna yako mwenyewe.
Kisha nikaacha kazi yangu nzuri ili nijikite kwenye biashara moja kwa moja.
Nikakutana na hasara za biashara, kampuni zilizoshindwa, usiku wa kufanya kazi, mikopo na wakati mwingine mustakabali ulioonekana kuwa wa giza. Safari ya kujenga biashara changa haileti maisha mazuri haraka haraka.
Katika hatua zote hizi, swali moja liliendelea kubaki kichwani kwangu:
Maisha mazuri ni yapi?
Unajuaje kuwa unaishi maisha mazuri?
Na unayapataje?
Maana yangu ya maisha mazuri iliendelea kubadilika. Ilitegemea nilipokuwa, kile nilichokosa na mahali nilipotaka kufika.
Lakini katika matumaini na maumivu yote, mambo machache hayakubadilika. Mambo hayo yaliendelea kuwa sehemu ya maisha niliyotaka kuishi.
Leo ninaamini ndiyo msingi wa maisha mazuri:
Afya njema.
Familia yenye utulivu.
Utajiri endelevu.
Mtu wa kumpenda.
Na jambo lenye maana la kufanya.
Afya Njema
Kutokuwa na afya nzuri, kusumbuliwa na magonjwa ni moja ya hali ngumu zaidi maishani.
Changamoto za kiafya huleta maumivu ya mwili, madhara ya kihisia na mateso ya kisaikolojia. Pia huweka shinikizo kubwa kwa familia yako, marafiki zako na hali yako ya kifedha.
Ninashukuru kwamba katika kukua kwangu sikuwa na matatizo mengi ya kiafya. Lakini miaka michache iliyopita, nilianza kusumbuliwa na maumivu makali ya tumbo.
Mwanzoni niligunduliwa kuwa na aina isiyo ya kawaida ya vidonda vya tumbo. Kilichofuata kilikuwa safari ndefu ya kutumia dawa, kwenda hospitalini na kubadilisha mtindo wangu wa maisha.
Nakumbuka mambo ambayo watu ninaowapenda walipitia walipokuwa wakijaribu kunisaidia. Nakumbuka idadi ya vidonge na dawa nilizotakiwa kutumia. Nakumbuka ni mara ngapi nilishinda hospitali tofauti tofauti.
Mpaka leo, inauma kukumbuka kiasi cha fedha nilichotumia nikijaribu kurejesha afya yangu.
Uzoefu huo ulinifundisha kuwa maisha mazuri lazima yaambatane na afya njema.
Kuna mambo mengi tunayoweza kufanya ili kulinda afya zetu. Tunaweza kula vizuri, kufanya mazoezi, kupumzika na kupata usingizi wa kutosha.
Mambo haya yanaonekana kuwa rahisi. Lakini mara nyingi tunayapuuza mpaka miili yetu inapotulazimisha kuyapa umuhimu.
Bila afya njema, inakuwa vigumu kufurahia mambo mengine yote. Bila afya njema hakuna maisha mazuri.
Familia Yenye Utulivu
Familia zenye utulivu zinazidi kuwa nadra.
Utamaduni wetu umeanza kuhama kutoka kwenye maisha ya kijamii na kifamilia kuelekea kwenye ubinafsi. Watoto wengi zaidi wanalelewa na mama au baba peke yao. Ndugu wanakua mbali na wenzao. Wazazi wanatumia muda mwingi kutafuta fedha au kujenga kazi zao kiasi kwamba hawawajui vizuri watoto wao wenyewe.
Kwa watu wengi, upendo wa kwanza na hisia ya kukubalika huanzia ndani ya familia.
Familia yenye utulivu inakupenda kabla dunia haijatambua thamani yako. Inajaza moyo wako upendo ili uweze kwenda nje na kuwashirikisha wengine upendo huo.
Nililelewa na mama peke yake. Madhara ya kukua bila baba bado yapo ndani yangu.
Mama yangu alifanya kila alichoweza kuwa kila kitu kwetu. Lakini hasingeweza pia kuwa baba yetu. Mtu mmoja hawezi kutimiza kikamilifu nafasi zote mbili, hata akijitahidi kiasi gani.
Huwezi kubadilisha familia uliyotoka.
Inaweza kuwa ilikuwa imara, haikuwa na utulivu au ilikuwa imevunjika kabisa.
Lakini unaweza kubadilisha namna unavyohusiana na familia yako leo. Unaweza pia kuamua aina ya familia unayotaka kuijenga.
Kama umetoka katika familia iliyovunjika, unajua mambo yaliyosababisha maumivu. Unajua kile kilichokosekana. Tumia mafunzo hayo kuepuka kuleta majeraha yaleyale katika familia yako.
Kama umetoka katika familia yenye utulivu, tayari una mfano wa kufuata. Umebahatika. Tumia hekima uliyoirithi.
Mafanikio mengi hupoteza maana pale unapokosa mtu wa kushirikiana naye.
Kuwa tajiri bila familia karibu kunaweza kuleta upweke. Kuwa maskini bila familia ya kukusaidia kunaweza kuleta maumivu.
Maisha mazuri yanahitaji familia. Muhimu zaidi, yanahitaji familia iliyojengwa juu ya upendo, uwepo na utulivu.
Utajiri Endelevu
Afya njema na familia yenye utulivu hujenga msingi imara. Lakini umaskini wa muda mrefu unaweza kuviharibu vyote viwili.
Umaskini hupunguza ubora wa chakula unachoweza kumudu. Unaathiri muda wako wa kupumzika, usingizi na uwezo wa mwili kujijenga upya. Unapunguza chaguo ulizonazo na kukufanya uishi ukifikiria tu namna ya kuvuka siku ya leo.
Umaskini unaweza pia kuingia kati ya familia na mahitaji yake. Kadiri muda unavyopita, shinikizo la kifedha linaweza kuharibu hata mahusiano imara.
Hakuna jambo zuri linalotokana na kubaki ndani ya mtego wa umaskini.
Maisha mazuri yanahitaji utajiri endelevu.
Hii haimaanishi lazima uwe tajiri kupita kiasi. Inamaanisha kuwa na uwezo wa kukidhi mahitaji yako ya msingi. Inamaanisha kuwa na akiba ya dharura na kujenga zaidi ya chanzo kimoja cha kipato.
Utajiri endelevu hukulinda wewe na familia yako dhidi ya hali zisizotabirika. Unakupa nafasi ya kusimama tena nyakati ngumu zinapokuja.
Na nyakati ngumu zitakuja.
Fedha peke yake haziwezi kutengeneza maisha mazuri. Lakini ukosefu wa fedha unaweza kuharibu mambo mengi yanayowezesha maisha mazuri.
Mtu wa Kumpenda
Kutokana na uzoefu wangu, nimegundua kuwa unaweza kuwa na afya njema, familia yenye utulivu na utajiri endelevu, lakini bado ukajisikia mpweke unapokwenda kulala.
Bado unahitaji mtu wa kushirikiana naye maisha na upendo wako.
Familia na marafiki ni muhimu. Lakini si kila mara wanaweza kuchukua nafasi ya kuwa na mwenza ambaye mnaweza kujenga familia na maisha ya baadaye pamoja.
Maisha mazuri yanajumuisha kuwa na mwenza anayekupenda, anayeshirikiana nawe katika maono yako, anayekuheshimu na anayekushangilia.
Unapotoka kwenda kupambana na dunia, unatakakiwa kurudi kwa mtu ambaye atakukumbatia. Mtu ambaye atasikiliza stori zako, atasherehekea ushindi wako na atakaa nawe wakati unaposhindwa.
Unataka mtu ambaye pia anaamini katika kujenga familia yenye utulivu kwa ajili ya watoto watakaoweza kuzaliwa katika uhusiano wenu.
Miongoni mwa vitu vitu vya muhimu kwenye hili ni kuchagua mwenza sahihi.
Kumchagua mwenza sahihi kuna maana kubwa zaidi ya sura, dini, elimu, rangi au utajiri. Mambo hayo yanaweza kuwa muhimu, lakini hayawezi kuubeba uhusiano peke yake.
Unapompenda mtu asiye sahihi, haijalishi utamfanyia nini au kusema nini. Siku zote utajisikia kuwa umekosea, hueleweki au hutoshi. Unaweza kufa kwa ajili yake na bado atasema haujafa vizuri.
Chagua kwa busara.
Mtu unayempenda ataathiri ubora wa maisha yako ya kila siku kuliko mtu mwingine yeyote.
Jambo Lenye Maana la Kufanya
Kuna wakati nilikuwa na ndoto za kustaafu nikiwa kijana na tajiri.
Niliwaza kuwa na fedha nyingi kiasi kwamba nisingehitaji kufanya kazi tena. Nilijiona nikilala kwenye fukwe nzuri za bahari, nikipiga kambi katika misitu ya kipekee na kutumia kila siku nikifurahia maisha.
Nilipoacha kazi yangu PwC, nilichukua mapumziko marefu. Nilitaka kuwa peke yangu na kutafakari kuhusu kile nilichotaka kufanya na maisha yangu.
Baada ya miezi miwili, niligundua kuwa kutofanya chochote kunachosha.
Nilijikuta nikiandika kuhusu maisha. Nilianza kusoma zaidi na kutengeneza vitu.
Baada ya PwC, nilirudi kwenye biashara na kufanya mambo mengi kwa ajili ya fedha. Kuna nyakati nilipata fedha nyingi. Lakini bado nilihisi kuwa kuna kitu kilikosekana.
Sikuhisi kuwa nilikuwa nafanya jambo lenye maana kwangu au kwa dunia.
Ndiyo maana niliendelea kuandika.
Nilikuja kuelewa kuwa sote tunahitaji jambo lenye maana la kufanya.
Kazi inayokupa maana maishani inaweza isiwe kazi ileile inayokujengea utajiri. Kama jambo moja linakupa maana na wakati huohuo linakujengea utajiri endelevu, wewe ni mmoja wa watu waliobahatika.
Watu wengi watafanya baadhi ya mambo ili kupata fedha na mambo mengine ili wajisikie hai.
Unaweza kujenga biashara siku za kazi na kuandika mwishoni mwa wiki. Unaweza kufanya kazi ofisini na kuitumikia jamii baada ya kazi. Unaweza kupata kipato katika eneo moja huku ukipata maana kupitia sanaa, kufundisha, michezo au imani.
Unapopata jambo linaloyapa maisha yako maana, usiliache.
Hii ni sababu mojawapo inayowafanya watu matajiri kuanzisha taasisi, kusaidia jamii zao na kuchunguza mambo wanayoyapenda. Baada ya kupata fedha, bado hutafuta jambo linalowapa maana.
Sote tunahitaji kujisikia kuwa tuna umuhimu. Tunahitaji kujua kuwa kuna sehemu yetu itabaki duniani hata baada ya sisi kuondoka.
Hitimisho
Nimejadili misingi hii kwa mpangilio unaoonekana kuwa wa kawaida kwangu. Pia ndiyo namna ninavyoamini mambo haya yanapaswa kupewa kipaumbele.
Lakini maisha mara chache hufuata mpangilio ulionyooka.
Kila mtu yupo katika safari tofauti. Tunasogea kwa kasi tofauti katika safari ya maisha.
Mtu anaweza kuwa amefika mbali katika kujenga utajiri lakini akawa anapambana na afya na familia. Mwingine anaweza kuwa na kazi yenye maana na fedha, lakini bado akapambana katika mapenzi. Mtu mwingine anaweza kuwa na familia yenye upendo lakini ana matatizo ya kifedha.
Usilinganishe safari yako na safari ya mtu mwingine.
Hii ni safari binafsi.
Jiangalie kwa makini na utambue ulipo. Tafuta sehemu ya maisha yako inayohitaji kupewa kipaumbele. Kisha chukua hatua. Haujachelewa.
Hakuna mwisho mmoja ambao kila mtu anatakiwa kuufikia katika umri fulani. Kuna maisha uliyonayo na maana yako binafsi ya kile kinachoyafanya yawe mazuri.
Mtu mmoja mwenye hekima aliwahi kusema:
“Fanya unachoweza, kwa kile ulicho nacho, pale ulipo.”
Mpaka wakati mwingine,
Uwe na furaha.
Uwe na afya.
Uwe na utajiri.
Watushule.

