Mahusiano ndiyo sehemu muhimu zaidi ya maisha, lakini pia ndiyo magumu zaidi kushughulika nayo.
Namna familia, marafiki na mahusiano ya mapenzi yanachangia mafanikio au matatizo
Mahusiano ndiyo sehemu muhimu zaidi ya maisha, lakini pia ndiyo magumu zaidi kushughulika nayo.
Kusini mwa Afrika, Ufalme wa Zulu uliinuka na kupata nguvu. Kufikia karne ya 19, upanuzi wake ulikuwa mkubwa sana kiasi kwamba uliwalazimisha baadhi ya makabila kuikimbia Zululand. Zwangendaba aliwaongoza watu wa Ngoni kutoka Zululand.
Aliwaongoza watu wake hadi Ziwa Tanganyika. Ziwa hili linapakana na Tanzania, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Burundi, na Zambia. Zwangendaba aliwaruhusu watu wake kuchukua maeneo ya makazi katika ukanda huo. Moja ya makundi hayo lilienda hadi kijiji cha Peramiho huko Songea, kusini mwa Tanzania.
Miongoni mwa watu waliohamia Peramiho alikuwemo kijana shupavu aitwaye Mphami Chitingili pamoja na kaka yake. Walipata wenza na kufunga na kuanzisha nao familia. Wakatengeneza marafiki na majirani huku wakilea familia yao.
Baada ya miaka kadhaa, wamisionari kutoka Ujerumani walikuja kwenye maeneo yao. Padre Cassian Spiss alianzisha Peramiho Abbey tarehe 31 Julai 1898. Alitoka katika shirika la Missionary Benedictines la mtakatifu Ottilien na alikuwa amewasili Afrika Mashariki mwaka 1888.
Kufikia mwaka 1910, utawala wa kikoloni wa Kijerumani ulikuwa umechukua udhibiti wa kijeshi wa Peramiho. Uwepo huo wa kijeshi pia uliimarisha uwepo wa wamisionari wa Kijerumani.
Wale waliopinga waliuawa au kulazimishwa kukumbatia utamaduni wa Kijerumani. Mphami alikuwa miongoni mwa wachache waliokimbia kijiji hicho ili kuukwepa ushawishi huo. Baada ya kuondoka katika eneo la wamisionari, aliingia katika jamii ya Kiislamu. Akasilimu na kuwa muislamu.
Watu wengine waliobaki waliingia chini ya udhibiti wa jeshi la Kijerumani. Nao wakaunganishwa kwenye jumuiya ya kimisionari, wakabatizwa na kuwa wakristo. Humo alikuwemo kaka yake Mphami, yeye akawa mkristo.
Kufikia katikati ya miaka ya 1900, familia ya Mphami ilikuwa imekua hadi kufikia watoto zaidi ya kumi, wajukuu zaidi ya thelathini, vitukuu zaidi ya sabini, na vilembwe wengi. Kaka yake Mphami naye alikuwa na familia ya ukubwa unaokaribiana na huo.
Mama yangu alikuwa miongoni mwa mamia ya vitukuu wa kike wa Mphami Chitingili. Ili mimi nizaliwe, ilihitajika mlolongo mgumu wa matukio kutokea kwa Mphami. Na yeye kuna vingi vilitokea mpaka kufika Peramiho kutoko kusini mwa Afrika.
Aliacha ndugu wengine, familia, marafiki, jamaa na majirani. Na huo ni upande mmoja tu wa historia ya familia yangu; hatuwezi hata kwenda ndani zaidi upande wa baba yangu.
Katika mchakato wa kujitambua, ilinibidi kuwaelewa wote ninaohusiana nao. Mbali na ndugu zangu wa tumbo moja, nina ndugu wengi upande wa baba na mama. Nina marafiki wengi niliowatengeneza kwa muda na mazingira tofauti. Nimewahi kupenda, kupendwa na kuwa kwenye mahusiano mengi ya kimapenzi pia.
Hiyo ndiyo njia aliyopitia Mphami Chitingili, na hiyo ndiyo njia ambayo kila mtu hupitia. Katika maisha yetu, tutajikuta tukiwa kwenye mahusiano mengi. Sisi ni sehemu ya familia fulani, na tutapenda au kuanzisha familia zetu wenyewe. Katika safari hii yote, pia tunapata ndugu na marafiki.
Sote tunaweza kukubaliana kwamba mahusiano ni muhimu zaidi maishani, lakini pia ndiyo magumu zaidi. Tunawahitaji watu ili kuishi vizuri, lakini watu pia ndio chanzo cha baadhi ya maumivu yetu makubwa sana.
Kwenye yale mambo muhimu matatu kwenye maisha, kazi, afya na mahusiano, hayo ya kwanza ya kazi na afya yanategemea sana mtu peke yake. Lakini mahusiano ni tofauti.
Yanamhusisha binadamu mwingine mwenye mahitaji, majeraha, matarajio, nafsi, kumbukumbu, na uhuru wake. Hilo ndilo linaloyafanya kuwa sehemu yenye maana zaidi maishani, lakini pia ngumu zaidi.
Watu waliomo katika maisha yetu wanaweza kuwa baraka zetu kubwa zaidi au mizigo yetu mikubwa zaidi. Lengo la makala hii ni kujadili vitu muhimu vya kujua na kuzingatia kwenye mahusiano yetu.
Kama ambavyo tulijadili kuwa vitu muhimu kwenye maisha vinakuja kwa tatu, basi na mahusiano pia yana nguzo tatu:
Familia, Marafiki, na Mapenzi
1. Familia
Familia ina ushawishi mkubwa kwa sababu ndio chimbuko la mahusiano yetu binadamu. Kabla haujajitambua na kujua maisha ni nini, unakuwa umechaguliwa kuwa kwenye familia.
Hadithi ya Mphami ilianza na familia yake. Sijui nini kilimtokea baba yake au ndugu zake wengine huko Zululand. Alihama pamoja na kaka yake. Mimi sikuwa na chaguo la kuwa sehemu ya ukoo wa Mphami kupitia kwa mama yangu. Mama yangu pia hakuchagua.
Kila mmoja wetu hakuwa na nafasi ya kuchagua familia aliyozaliwa ndani yake. Hata hivyo familia ndio inatengeneza msingi wa kwanza wa namna tunavyoiona dunia.
Familia inatengeneza misingi mikuu miwili ambayo mara nyingi inakuwa nasi mpaka mwisho wa safari yetu hapa duniani.
Kwanza, tunajifunza na kufyonza imani muhimu za maisha, kama vile dini, mitazamo ya kisiasa, fedha, na maadili. Wanafamilia wote waliotokana na Mphami walikuwa Waislamu. Aliikubali imani hiyo na akawalea katika njia hiyo. Wanafamilia wote waliotokana na kaka yake Mphami waliishia kuwa Wakristo.
Mimi nilizaliwa na wazazi wa dini tofauti: mama yangu akiwa Mwislamu na baba yangu akiwa Mkristo. Lenzi yangu ya kuutazama ulimwengu si sawa na ya wale waliozaliwa na wazazi wawili Wakristo au wawili Waislamu.
Asili za kitamaduni pia huunda mtazamo huo. Watu waliokulia nje ya Uislamu au Ukristo huutazama ulimwengu kwa mila na desturi tofauti. Kabla ya kukubali dini mpya, Mphami na kaka yake walifuata imani za jadi za Kizulu zilizokuwa za kawaida kwa familia za kusini mwa Afrika.
Watu wa bara la Asia wengi hawafuati ukristo wala uislamu, wahindi na waarabu wengi wana imani zao pia. Hii ni kwasababu walizaliwa kwenye familia zinazofuata mila, tamaduni na desturi zao. Na wengi huishi maisha yao bila kubadilisha.
Wengi wetu hufuata dini tuliyofundishwa na familia zetu, na mara nyingi imani hizo hubaki nasi maisha yote. Hilo linaweza kutufanya tuwahukumu wale wasioshiriki dini yetu na kuwaunga mkono wale wanaoshiriki imani yetu.
Hali ni ileile kwa siasa. Ikiwa familia yako ilikuwa inapenda chama fulani cha kisiasa au wazo fulani, kuna uwezekano mkubwa nawe ukashikamana nalo maisha yote.
Kama unatoka katika familia tajiri, utakuwa na mtazamo tofauti kuhusu fedha. Unaweza kuamini kwamba watu wanaweza kutumia fedha kufanya mema katika jamii. Huenda una ujuzi, uzoefu, na maarifa kuhusu namna ya kupata fedha, kuzisimamia, na kuzikuza.
Kama ulikulia katika familia yenye matatizo ya fedha, unaweza kuamini kwamba matajiri wengi ni waovu. Unaamini kwamba fedha ndiyo chanzo cha maovu yote. Kwa hiyo, huenda ukakosa ujuzi na uzoefu wa kutafuta, kuhifadhi, na kukuza fedha. Unakuwa katika mzunguko usioisha wa kuhangaika.
Kama ulikulia katika familia iliyovunjika au nyumba isiyo na furaha, kuna uwezekano mkubwa ukaumba hali kama hiyo baadaye maishani. Hautazami familia na maadili yake kama wale waliokulia katika familia imara.
Haukuwa na chaguo la familia yako, imani zao za dini, siasa, mtazamo kuhusu fedha na mahusiano. Ila una uwezo wa kuchagua zipi zimekusaidia, zipi hazina mashiko na zipi unataka kwenda nazo kwenye familia unayotengeneza.
Tafuta maadili kwa watu wengine na katika familia zao yanayokutia hamasa. Anza kuyaingiza katika maisha yako mwenyewe. Bado haujachelewa. Usipofanya hivyo, utarudia kutengeneza familia kama uliyotoka ndani yake.
Pili, familia zetu hutuwekea matarajio yaliyoundwa na historia zao na drama zao. Kila mtu mwenye jina la ukoo kama lako anaamini kuwa ana haki na jambo la kusema kuhusu maisha yako.
Wengi wetu hubeba mizigo bila hata kusimama kujiuliza kwa nini tunaibeba. Hatuangalii shinikizo hizo za kifamilia. Badala yake, tunaendelea mbele huku tukibeba mizigo isiyotuhusu.
Nina shangazi ambaye kila mara ananiuliza nitaoa lini. Wakati huohuo, binti yake ndoa yake haijadumu zaidi ya miaka mitano. Lakini bado anahisi ana haki ya kuniambia namna ya kuishi maisha yangu.
Nina binamu wa mbali. Anafikiri ninapaswa kumsaidia kupata kazi na kuwahudumia watoto wake aliowapata bila mpango kwa sababu tu wote tuna jina la ukoo moja. Nina ndugu ambao wana roho mbaya na wabinafsi, na wanategema niwe mvumilivu kwao kwa sababu tu eti“damu ni nzito kuliko maji.”
Sote hubeba mizigo hii katika maisha yetu yote. Lakini ili kuishi maisha mazuri, tunahitaji kusimama na kuishusha. Lazima tuchague kwa busara ni mizigo na matarajio gani tuyahifadhi na yapi tuyatupilie mbali.
Unahitaji kuweka mipaka kwa kila mtu katika familia na ukoo wako. Ni maisha yako, kwa hiyo unaweza kumwambia mtu yeyote hapana. Hilo linawahusu hata wazazi wako au hata yule bibi pale mtaani anayesema kuwa ni bibi yako kwasababu yeye alisoma na bibi yako shule ya msingi. Haujawahi kumuona maishani, lakini anategemea umtunze na kumjali.
Familia haziweki shinikizo, matarajio, au madai kwa mtu ambaye hafanyi chochote kikubwa. Wanadai vitu hivyo kwa sababu kuna jambo fulani linaendelea katika maisha yako. Mara tu jambo hilo linaposimama, unapoteza umuhimu kwao.
Sote tunawajua wanafamilia ambao hawaalikwi kwenye matukio. Hawapewi kipaumbele na hawaulizwi kuhusu chochote. Usiposimama na kuishusha mizigo yako, siku moja hautabaki na chochote, na hautakuwa tena na nafasi ndani ya familia.
Ndugu ambao walikuwa wanaomba misaada kwa baba aliyekuwa na kazi, biashara na uwezo kiuchumi ndio ndugu hao hao ambao huenda mahakamani kudai mirathi ya familia ya baba aliyefariki.
Kaka na dada ambao wanadamu nzito kuliko maji ndio hao wanaogombania mali za wazazi, wengine wanafikia hatua ya kuuana.
Njia bora ya kushughulika na familia na ndugu ni kuwa wa makusudi na mipaka.
Kuwa wa makusudi kuhusu muda, rasilimali, na nguvu unazowapa. Usishughulikiane nao kwa sababu tu ni wanafamilia na mna jina moja la ukoo. Shughulikiana nao kwa sababu ni watu wazuri wanaokujali, na wewe pia unawajali. Unafurahia kuwa pamoja nao.
Ni muhimu kujijenga kwanza wewe binafsi ili uwe na uwezo wa kuwajenga wengine. Hauwezi kutoa msaada ambao hauna kwa sababu ya matarajio ya watu. Usikubali kubeba mizigo ambayo haikuhusu kwa sababu damu ni nzito kuliko maji.
2. Marafiki
Kumbukumbu yangu ya kwanza ya marafiki ni Ibrahim, Robert, na Elisha nilipojiunga na chekechea. Nakumbuka baadhi ya vituko vya usumbufu tulivyokuwa tukivifanya wakati wa mapumziko ya chakula cha mchana. Baadaye tuliungana pamoja katika Shule ya Msingi St Joseph’s.
Nimekutana na marafiki wengi katika hatua tofauti za maisha, kuanzia shule ya msingi na chuo kikuu hadi sehemu mbalimbali za kazi. Wengine niliwapata kupitia mpira wa miguu, na wengine kwenye mitandao ya jamii.
Na pia nimepoteza marafiki wengi maishani. Nilipoteza mawasiliano na marafiki mara tu tulipomaliza shule au chuo kikuu. Nilipoteza uhusiano na wengi nilipoacha tu kazi. Nilipoteza marafiki niliowapata kwa sababu nilibadilisha sehemu ya kuishi, Nimewapoteza wengine kwa kifo.
Marafiki tofauti katika hatua tofauti za maisha walinijenga kuwa nilivyo. Baadhi yao walinijengea mazoea mazuri, msukumo, hekima, na roho ya kuthubutu. Wengine walikuwa washawishi wakubwa wa tabia zangu zote mbaya nilizozijenga.
Sote tunakusanya marafiki tofauti katika hatua tofauti za maisha. Urafiki ni mahusiano ya pekee kwa sababu ni familia tunayochagua. Hata hivyo, pia ni familia ambayo tunaweza kuiachia kwa urahisi zaidi kuliko ndugu zetu wa damu pindi njia zetu zinapotofautiana.
Utafiti unaonyesha kwamba kila mtu, katika umri wowote, huwa na marafiki wachache tu wa kweli. Hao ni watu watakaokuwapo unapowahitaji, watasherehekea ushindi wako, na kuhisi maumivu yako.
Ni muhimu kuwatambua hao marafiki wako wachache na kujitahidi kuwa rafiki mwema kwao. Kuna mtu aliwahi kusema kuwa binadamu anakuwa na tabia zinazoendana na wastani wa watu watano wanaomzunguka.
Tambua marafiki zako wa kweli watano na wekeza nguvu kwao. Kujuana na watu wengi haimaanishi una marafiki wengi. Ukipata shida kwenye maisha una watu chini ya watano ambao watakua tayari kuhangaika na wewe usiku na mchana. Ukiwa na mafanikio utapata watu hata kwa maelfu.
Pia usichanganye watu unaojuana nao au unaofanya nao kazi na kuhisi hao ni rafiki zako. Hao ni wafanyakazi wenzako. Wote mpo hapo kutafuta riziki sio marafiki. Ikitokea inabidi wachague wewe na kazi unajua watakachochagua, kwasababu na wewe ungefanya hivyo pia.
Kudumisha urafiki kunahitaji uwe wa makusudi. Mnahitaji kuwasiliana mara kwa mara. Mnahitaji kupata muda wa kukutana na kuzungumza. Unahitaji kuwapo kwa ajili yao katika nyakati zao za raha na shida.
Ukifikiri kwamba wewe ndiye wa muhimu zaidi katika urafiki, watu wataona. Na polepole wataanza kujitenga na wewe. Hakuna mtu anayetaka kuwa mwigizaji wa pembeni katika hadithi yako ya maisha yenye ubinafsi.
Usidanganyike na kujifanya muhimu sana kwa marafiki. Kila siku wao ndio wakutafute wewe. Kila siku wao ndio wasapoti biashara yako, malengo yako na ndoto zako. Kila siku wao ndio wakutembelee. Urafiki ni majukumu ya pande mbili.
Marafiki wa kweli hawajali kama wewe ni tajiri au maskini. Hawajali kama una cheo kikubwa au kidogo. Hawajali kama wewe ni maarufu au la. Hawajali kama una sura nzuri au la. Wataishi na wewe kwa namna ileile na watakuwa waaminifu kwako. Na wewe pia unapaswa kufanya vivyo hivyo.
Marafiki bora ni wale uliowapata wakati hauna kitu, una matatizo na unapitia shida. Marafiki bora ni wale uliowatengeneza utotoni, shuleni au chuoni. Marafiki bora ni wale wanaokujua wewe nje ya mitandao ya jamii.
Unavyozidi kuzeeka, ndivyo inavyokuwa vigumu zaidi kupata marafiki wazuri na wa kweli. Jifunze kushikilia urafiki uliojenga tangu utotoni. Ni vigumu kuwabadilisha marafiki wa kweli wa muda mrefu.
3. Mahusiano ya kimapenzi
Mara ya kwanza nilipohisi kuvutiwa na mtu ambaye hakuwa familia wala rafiki nilikuwa na umri wa miaka kumi na miwili. Kulikuwa na msichana mmoja aliyehamia katika shule yetu ya msingi St Joseph. Nilijikuta nikihisi kutokuwa sawa akiwa karibu nami.
Alipokuwa karibu, nilijikuta nikikosa maneno. Niligundua nilikuwa na aibu zaidi, kimya zaidi, na tofauti. Kwa kawaida nilikuwa naongea sana, matani na mizaha mingi mno. Lakini nikiwa karibu naye, yote hayo yalitoweka. Pia niligundua nilikuwa nampa kila alichoniomba: vitabu, daftari, kalamu zangu, na hata chakula changu wakati mwingine.
Wakati huo, sikujua mapenzi ni nini, hivyo nilihisi ni aina fulani tu ya urafiki kwa mwanamke. Tulipomaliza shule ya msingi na kila mmoja kwenda njia yake bila mimi kukiri hisia zangu, niligundua kuwa yale ndio mahaba.
Miaka imepita sasa; nina uzoefu wa kupenda na kupenda. Nimejifunza kwamba unaweza kumpenda mtu, na kutaka kuwa naye muda wote. Pia nimejifunza kwamba unaweza kumpenda mtu na usitake kabisa kuwa na jambo lolote na yeye.
Watu wanaanzisha mahusiano ya kimapenzi kwa sababu tofauti. Wengine huhisi vipepeo visivyoelezeka tumboni wanapokuwa karibu na mtu fulani. Wengine huvutiwa na muonekano wa watu.
Kwa baadhi, ni kwa sababu watu hao huwafanya wajisikie wa pekee. Kwa wengine, ni kwa sababu wametumia muda mwingi nao kiasi kwamba wameambatana nao kihisia.Wengine huingia kwa sababu familia au jamii imepanga hivyo.
Katika maisha yangu, nimejifunza kwamba namna unavyoanza uhusiano wa kimapenzi si jambo muhimu sana. Muhimu ni nani unaanza naye mahusiano na unafaya vitu gani kwenye hayo mahusiano.
Watu wawili hujenga mahusiano wa kimapenzi. Kadiri kunavyokuwa na mwingilio mdogo kutoka kwa wengine—ikiwemo familia, marafiki, na wenzangu wa kazi—ndivyo ilivyo bora zaidi.
Kama watu wawili walio kwenye uhusiano hawana msimo na maamuzi ya pamoja basi msingi mzima wa mahusiano yao unakuwa ni dhaifu.
Mtazamo wangu kuhusu mahusiano ya kimapenzi unaweza kufupishwa katika mambo matatu:
Jambo la kwanza ni kumkubali mwenzako kama alivyo. Binadamu tumeumbwa tofauti, tumelelewa tofauti na tumepitia maisha tofauti. Na mpenzi wako naye ni hivyo hivyo. Kumpenda au kukupenda wewe haifanyi yeye aache kuwa tofauti.
Mpenzi wako haioni dunia kama unavyoiona wewe. Familia yake ilimpa mitazamo na malezi tofauti na wewe. Marafiki zake wamemjengea tabia tofauti na zako. Mahusiano yake yaliyopita yalikuwa na watu tofauti na wewe. Kama ambavyo wewe ni wa utofauti na yeye.
Hiyo ina maana kwamba haoni ulimwengu kama wewe unavyouona. Hawezi kuwa kama wewe. Hakuna tatizo lolote kwa mtu mwingine kuwa tofauti. Wewe unaweza kuona sita na yeye akaona tisa katika hali ileile, na huenda nyote wawili mkawa sahihi.
Kukubali tofauti za mwenza wako kutakusaidia kumthamini na kumpenda kwa jinsi alivyo. Kushindwa kufanya hivyo ni mafuta ya mabishano yasiyo ya lazima, drama, na mateso.
Pili, kila mwenza lazima ajifunze jinsi ya kuwasiliana na mwenzake. Kila kitu maishani hurudi kwenye mawasiliano. Nchi huingia vitani kwa sababu ya mawasiliano mabovu, na nchi huunda ushirikiano kwa sababu ya mawasiliano mazuri.
Mawasiliano mazuri huleta amani kwa wenzi wa kimapenzi, lakini mawasiliano mabovu huleta migogoro. Kujua nini cha kusema, wakati gani wa kusema, na namna gani ya kusema ni jambo la msingi sana. Hilo humsaidia mtu mwingine ajisikie kuheshimiwa, kupendwa, na kutunzwa.
Kama una mpenzi ambaye hajui muda wa kuongea, muda wa kukaa kimya, muda wa kuomba msamaha basi kuna shida kubwa sana. Kama wewe haujui kitu gani cha kusema mbele za watu na kitu gani cha kusubiri mkiwa wawili basi una changamoto.
Jambo la tatu ni kwamba mahusiano ya kimapenzi hayapo ili kumkamilisha mtu yeyote. Hili huenda likawa jambo muhimu zaidi. Hauingii kwenye mahusiano ukiwa umevunjika ukitarajia mwenza wako akukamilishe au akurekebishe. Wala wewe si mkamilifu kiasi cha kumrekebisha mwenza wako au kumkamilisha.
Kauli kama “mke akiwa na furaha, ndoa na maisha huwa na furaha” ni uongo tu. Unahitaji mtu mwenye furaha ili kujenga maisha yenye furaha. Ikiwa mume hana furaha, hakuna kitu atakachoweza kumpa mke wake ili awe na furaha. Mume asiye na furaha anapojaribu kumfurahisha mke wake, hiyo ni tiketi ya majanga.
Ni muhimu kujijenga wewe na kuwa bora ili uweze kulete ubora kwenye mahusiano. Hauwezi kumsaidia mtu anayezama kama haujui kuogelea. Jifunze kuwa na furaha ukiwa peke yako, na utaumba mazingira ya furaha pamoja na mwenza wako.
Jifunze kujitegemea mwenyewe kwanza kabla ya kutegemewa na mwenza wako. Jifunze kujipenda mwenyewe kabla haujatoa upendo kwa mtu. Jifunze kujijali mwenyewe kabla haujaanza kumjali mtu.
Ukimpata mwenza ambaye na yeye ana furaha akiwa peke yake, anajitegemea, anajipenda na kujithamini basi atakuja kwenye mahusiano akiwa bora zaidi na mahusiano yatakuwa na nafasi kubwa ya kukua.
Ingawa nimesema kumkubali mwenzako kama alivyo, kujua namna bora ya kuwasiliana na kuhakikisha hauendi kwenye mahusiano ukitegemea mwenza wako akukamilishe bado kuna kitu kimoja muhimu zaidi;
Ni lazima uchague mtu sahihi wa kuingia kwenye mahusiano. Sio kila mtu ni sahihi kwa ajili yako. Mtu anaweza kuwa sahihi kwa wazazi, marafiki, majirani au mitandao ya jamii lakini sio sahihi kwako.
Ukiwa na mtu ambaye sio sahihi kwenye mahusiano haijalishi utafanya nini, hamna utakachopatia na hamna mtakapofika. Unaweza kufa kwa ajili ya hayo mahusiano na bado utaambiwa haujafa vizuri.
Tumeangalia kwa undani nguzo tatu za mahusiano; familia, marafiki na mapenzi. Na tumeweza kujadili baadhi ya vitu vya muhimu sana kujenga mahusiano bora ili kutengeneza msingi wa nguzo ya maisha ya mahusiano.
Mahusiano yako yakiwa imara, basi kazi na afya yako nayo itakuwa kwenye nafasi nzuri zaidi ya kuwa imara.
Binadamu kwa asili ni viumbe wa mahusiano. Hakuna anayekuwa mtu akiwa peke yake. Uzuri wa mahusiano ndiyo pia unaoyafanya yawe magumu. Mahusiano ni muhimu kwa sababu yana uhai. Hubadilika. Yanahitaji msamaha, subira, mawasiliano, kujitoa, na ukomavu.
Maumivu mengi ya mahusiano hayasababishwi na chuki, bali na kutokomaa. Watu huumizana kwa sababu ya kiburi, ubinafsi, mawasiliano mabovu, kutokujiamini, majeraha ya zamani, na matarajio yasiyo halisi.
Maisha mazuri hayajengwi kwa kukwepa ugumu wa mahusiano, bali kwa kujifunza namna ya kuyashughulikia vizuri. Lengo si kuwa na mahusiano makamilifu. Lengo ni kuwa na mahusiano sahihi kwako.
Safari yangu ilianza muda mrefu kabla ya Mphami Chitingili kutoka Zululand huko Afrika Kusini, na sasa niko hapa pamoja nawe. Huenda unasoma haya ukiwa mwanafamilia, rafiki, mwenzangu wa kazi, jirani, mpenzi, mpenzi wa zamani, au mtu ambaye tulikutana naye mtandaoni.
Najua kuwa mimi nikiwa bora, basi nitakuwa na mahusiano bora kwako. Na wewe ukiwa bora, utakuwa na mahusiano bora na mimi. Na hii ndio njia sahihi ya kujenga mahusiano yako yote, na familia, marafiki na mapenzi.
Makala itakayofuata tuaangalia msingi wa pili wa maisha, afya. Tutaangalia afya ya mwili, akili na roho. Tutaangalia jinsi afya duni inavyoweza kupunguza sana ubora wa maisha yako na kuzuia uwezo wako.
Panapo majaaliwa
Fikiri kwa kina, Ishi kwa makusudi.
Watushule

