Kuwajua watu wengi kwa karibu haiwafanyi wote kuwa ni wa muhimu kwako.
Kanuni ya Pareto inasema mambo mengi ya muhimu hutengenezwa na mambo machache sana. Hivyo pia kwenye kazi, afya, fedha na mahusiano.
Asilimia Ishirini Inayobeba Maisha Yako
Nina mdogo wangu wa kike. Nampenda sana. Lakini kwa miaka mingi, uhusiano wetu ulinisumbua.
Ni mpole, ana akili na mchangamfu sana. Ana nyota ya kuingia sehemu na watu wakafurahia uwepo wake kwa haraka sana. Shida yake ni kuwa baada ya muda anatoweka.
Unatuma ujumbe. Hakuna jibu. Wiki mbili zinapita. Mwezi mmoja unapita. Kisha kuna siku anarudi — na wakati anaporudi, ni mambo mawili tu: inawezekana mambo mabaya yamemkuta au kuna vitu vizuri sana vinaendelea kwenye maisha yake. Hakuna kitu kati ya hayo.
Niliongea naye mara nyingi sana. Hakuna kilichobadilika. Mwaka jana niliamua kumuelezea ukweli wote, nikamwambia: unatoweka, kisha unarudi kana kwamba hakuna kilichotokea. Unajua maumivu ambayo unasababisha?
Akatabasamu kidogo, akasema: “Bro, mimi nina watu wengi maishani mwangu. Lakini nina watu wachache sana wa muhimu. Nawe uko miongoni mwa wale wa muhimu zaidi.”
Sikujua nifanye nini na maneno hayo. Sikujua nifikirie nini.
—
Labda hakuwa anaelewa kasoro yake. Labda alikuwa anaelezea kanuni ya maisha.
Kuna aina mbili za watu katika maisha yako. Watu wa karibu. Na watu wa muhimu. Watu wa karibu wapo katika maisha yako ya kila siku — unakula nao, unapiga nao stori, mnatumiana vichekesho kwenye mitandao ya jamii.
Watu wa muhimu ni tofauti kabisa. Wanabadilisha jinsi unavyofikiri. Unawakumbuka hata wakiwa mbali. Unawatafuta wakati maisha yanakuumiza au yakikufurahisha. Ni watu ambao unajua wapo kwa ajili yako utakapowahitaji, na wewe utakuwa kwa ajili yao watakapokuhitaji.
Watu wengi wanachanganya hizo aina mbili. Lakini si sawa.
Nilipopata ufahamu huo, nilianza kuuona kila mahali. Katika biashara. Katika fedha. Katika afya. Katika ujuzi. Mfumo ule ule, uliojificha chini ya vitu vya kawaida kabisa.
—
Hii inaitwa Kanuni ya Pareto — au kwa lugha ya kawaida, sheria ya asilimia themanini kwa ishirini, 80/20.
Vilfredo Pareto alikuwa mwanauchumi maarufu. Aligundua kitu cha ajabu bustanini mwake — asilimia themanini ya mbaazi zake zilitoka kwenye asilimia ishirini tu ya maganda.
Akaangalia umiliki wa ardhi nchini Italia. Mfumo ule ule. Asilimia ishirini ya watu walikuwa wanamiliki asilimia themanini ya ardhi yote. Aliendelea kutafuta. Uwiano huo ukiendelea kuonekana, tena na tena.
Asilimia themanini ya matokeo yanatoka kwenye asilimia ishirini ya juhudi. Maisha hayapo sawa. Hayajawahi kuwa sawa. Mgawanyo wa vitu daima umekuwa si sawa — na watu wanaojua hilo wanaacha kutafuta usawa.
Badala yake wanauliza swali moja tu: asilimia ishirini ipi ya kwenye maisha yangu inaleta asilimia themanini ya mahitaji, ndoto na malengo yangu?
KATIKA MAHUSIANO
Unaweza kuwa na watu kumi unaowaita wa karibu. Lakini wawili tu kati yao ndio wa muhimu — wale wanaobadilisha maamuzi yako, wale unaowapigia simu wakati mambo yanakuangukia, wale wanaokujali na kukuthamini kwa hali uliyokuwa nayo.
Usitegemee kila uhusiano kubeba uzito sawa. Weka uwekezaji wako wa kweli kwa wale asilimia ishirini wa muhimu. Waache wengine wawe walivyo.
Asilimia ishirini ya watu wanafanya maisha yawe mazuri au mabaya. Asilimia ishirini ya watu wanakusababishia asilimia themanini ya maumivu ya kichwa au furaha ya moyo. Watambue. Ishi nao kwa akili.
KATIKA BIASHARA
Biashara inaweza ikawa na bidhaa themanini na kuamini kila moja ina uzito sawa. Lakini ukweli ni huu — bidhaa moja au mbili ndizo zinazoleta asilimia themanini ya mapato. Zilizo nyingine ni kelele tu.
Ofisi moja inaweza kuwa na wafanyakazi hata mia, lakini asilimia ishirini tu ya wafanyakazi hao ndio wanoingiza asilimia themanini ya mapato na faida kwenye ofisi.
Biashara zinazokua haraka ni zile zinazogundua kanuni hiyo mapema. Zinawekeza kila kitu ndani yake. Nguvu inayotumika sehemu moja inakuwa. Nguvu iliyotawanyika inapoteza uwezo wake wa kuleta matunda.
Jiulize sasa hivi: bidhaa ipi, mteja yupi, njia ipi ya uuzaji ndiyo inayobeba zaidi? Kisha jiulize muda wako wa kweli unakwenda wapi. Jibu hilo litakuambia kila kitu.
KATIKA FEDHA
Watu wengi wanapigia mahesabu ya pesa zao kwa kuogopa kila kitu kwa wakati mmoja. Bili ya umeme. Akaunti ya akiba. Pesa za matumizi ya chakula au nauli Kila kitu, kwa uzito sawa, kwa wakati mmoja.
Lakini ukweli ni huu — maamuzi machache ndio yanayoamua maisha yako yote ya kifedha. Kuanza kuweka akiba mapema. Kuepuka madeni yenye riba kubwa. Kupunguza matumizi mabaya na yasiyo na lazima.
Kama una matatizo ya pesa kila wakati, kuna asilimia ishirini ya matumizi yako inayosababisha asilimia themanini ya matatizo yako ya kifedha. Yatambue. Yashughulikie.
KATIKA AFYA
Unaweza kutumia pesa kwa dawa, matibabu, na mitindo mingi ya maisha ya kisasa. Au unaweza kutafuta mambo mawili au matatu yanayobadilisha afya yako kwa kweli — usingizi, mazoezi, chakula unachokula — na kufanya hivyo kwa uthabiti na uvumilivu.
Utafiti unaonyesha mara nyingi sana kwamba tabia chache ndizo zinazozalisha matokeo mengi ya afya. Kila kingine ni marekebisho tu.
Asilimia ishirini ya mfumo wako wa miasha ndio unaleta asilimia themanini ya matatizo ya kiafya ya watu. Vyakula, vinywaji na kutokufanya mazoezi vinaleta magonjwa mengi kushinda kitu chochote.
Na watu wanaoweza kurekebisha mfumo wao wa maisha kwenye vitu hivyo wanabadilisha afya yao kuwa bora kwa asilimia themanini.
—
HITIMISHO
Mdogo wangu aliniletea maumivu mengi sana kwa muda mrefu kwamile tabia yake. Lakini upande wa pili wa maumivu hayo, nilijifunza kitu kuhusu kanuni ya ufanisi wa Pareto.
Si kila mtu anayekupenda atakuwa karibu kila wakati. Si kila bidhaa utakayo itengeneza itakuza biashara. Si kila ujuzi unaomiliki utabadilisha maisha yako. Si kila tabia utakayoijaribu itakusogeza mbele. Sio kila rafiki uliyenaye atakuwepo wakati wa shida.
Lakini daima kutakuwa na asilimia ishirini. Na asilimia hiyo ishirini ndiyo itakayokuwa na jukumu kubwa katika kubadilisha maisha yako.
Jukumu lako ni kutambua asilimia ishirini inayibadilisha sehemu za maisha yako na kuweka juhudi kwenye hizo.
Panapo majaaliwa..
Watushule

