Kutokuwa na ugonjwa haimaanishi una afya njema
Afya njema inahitaji mwili, akili na nafsi yenye amani
Ilikuwa siku ya kuzaliwa ya mwanamke mmoja mwenye uchangamfu mkubwa, aliyekuwa ametimiza miaka mia moja. Tangu nimfahamu, siku zote alikuwa akichanganya tarehe yake ya kuzaliwa, hivyo tuliendelea tu kukubali siku yoyote ambayo alikuwa anapendekeza.
Anna alikuwa ametimiza miaka mia moja lakini bado alikuwa mwenye nguvu na mwenye hekaheka sana. Siku ya kuzaliwa kwake, aliandaa chakula cha watu wanne. Alisimama kwa muda mwingi wa sherehe na hata akatuonyesha namna anavyochezaga kanisani.
Kwa udadisi, nilimuuliza ni nini kinachomfanya awe na afya nzuri hivyo wakati ana miaka mia. Alitabasamu na kutazama angani. Kisha akasema, “Mimi ni binti mpendwa zaidi wa Mungu.” Sote tukacheka. Ilikuwa ni jibu la utani lenye ujanja ujanja kutoka kwake.
Kwa muda wote ambao nimemfahamu, amekuwa akilima shamba lake na kufuga kuku. Alikuwa maarufu kwa kutembea kila mahali. Iwe anaenda shambani, kanisani, kuchota maji, au kutembelea majirani, siku zote alikuwa akitembea.
Alijulikana kwa kuwa wa kwanza kufika kanisani kila asubuhi. Alikuwa kanisani kila Jumapili.
Nakumbuka stori yake na namna alivyohamia eneo hili. Eneo hili hili ambalo leo tulikuwa tunasherehekea siku yake ya kuzaliwa. Alisafiri kutoka Tabora, akivuka zaidi ya kilomita 760 hadi kufika Kigamboni, Dar es Salaam, kuanzisha maisha yake mapya.
Aliacha kazi ya ualimu Tabora na kuja kujikita katika kilimo na ufugaji katika eneo hilo. Sasa Kigamboni ni mji wenye mipango ya kufanywa satellite city, lakini alipokuja, palikuwa ni pori. Zamani ilikuwa ukifika sehemu unaweka alama na mipaka na pori linakuwa lako.
Alitupikia chakula kwenye siku yake ya kuzaliwa kutimiza miaka mia moja. Haikuwa chakula cha kifahari; kilikuwa ni chakula chake cha kawaida alichokipenda kila siku. Alitupatia viazi vitamu vya kuchemsha kwa ajili ya chai, vilivyolimwa kwenye shamba lake mwenyewe.
Kwa chakula cha mchana, alitupatia wali na maharage. Vitu vyote alivitoa shambani kwake na akavipika katika jiko lake la nje. Sisi tulileta soda na vitafunwa, ambavyo hakuvipenda.
Anna, bibi yangu upande wa baba, alifariki miaka mitatu baadaye, miezi michache baada ya kutimiza miaka 103. Walinichagua mimi kusoma wasifu wake wa mazishi kwenye msiba. Kila mtu aliamini mimi ndiye nilikuwa mjukuu wake pendwa zaidi.
Baada ya kusoma wasifu na kutoa hotuba yangu fupi, nilikumbuka swali nililomuuliza miaka mitatu iliyopita kwenye siku yake ya kuzaliwa ya mia moja: “Siri yako ya maisha yenye afya ni nini?”
Wakati ule nilihisi jibu lake la “Mimi ni binti mpendwa zaidi wa Mungu” lilikuwa la kawaida tu, lakini lilibaki moyoni mwangu. Nilifanya utafiti kuhusu afya na nikagundua kwamba matatizo ya zamani zaidi mara nyingi huwa na suluhisho zilizojaribiwa na kuthibitishwa na wakati.
Ninaamini mambo bora zaidi maishani huja kwa namna ya tatu. Nafikiri maisha yenye afya sawa yanahitaji uwiano kati ya mwili, akili na roho. Mawazo haya yanatokana na uzoefu wa bibi yangu na watu wengine duniani wanaozeeka vizuri.
Mwili
Mwili ni chombo kinachobeba maisha. Mwili dhaifu hubeba maisha dhaifu; mwili wenye nguvu hubeba maisha yenye nguvu. Bibi yangu alikuwa na nguvu sana kwa mwanamke wa miaka mia moja. Bado angeweza kutembea kwenda kanisani, kupika, kucheza na kusimama kwa saa nyingi.
Nilijifunza mambo matatu muhimu kutoka kwa bibi yangu kuhusu mwili: jinsi alivyokuwa akitembea na kuufanyisha mwili wake, kile alichokula, na namna alivyokuwa anapumzika.
Mwili usiofanya kazi na mazoezi huwa dhaifu
Kibaiolojia, kiungo ambacho hakitumiki mara kwa mara au hakitumiki ipasavyo hudhoofika. Miili yetu imeumbwa kusogea na kufanya kazi. Kuanzia seli za ubongo hadi vidole vya miguu, kuna mfumo ambao mwili unatakiwa ufanye kazi.
Kuusogeza mwili na viungo huongeza mzunguko wa damu, nguvu, mchakato wa uchomaji wa chakula mwilini, mkao wa mwili, uwezo wa kusogea, nguvu za mwili, na hata hali ya moyo.
Bibi yangu alitembea sana. Kama angekuwa na saa ya kisasa ya kuhesabu hatua, ningeweka dau kuwa angekuwa anazidi hatua 10,000 kila siku kwa miaka mingi. Alikuwa anatembea au anazunguka au anafanya shughuli iliyokuwa inahitaji mwili kufanya kazi karibu muda wote tangu aamke hadi alale.
Mara nyingi alitembea huku amebeba mizigo, kama ndoo za maji ya kuogea, chakula cha kuku, vyombo vya kuosha, au mazao ya kuleta nyumbani kutoka shambani.
Alikuwa anaupa mwili kazi sana. Alikuwa akiinama kuokota vitu, akicheza kanisani, akinyoosha mikono kuchuma matunda, na akipiga magoti wakati wa kupika.
Shughuli hizi zote ziliusaidia mwili wake kubaki imara, wenye kunyumbulika, na wenye uwezo wa kutembea bila fimbo ya kutegemea hata alipokuwa na miaka mia moja.
Mtindo wake wa maisha ulimlazimisha kuwa na aina hizi za mizunguko na kuupa mwili kazi. Mtindo wa maisha wa mababu zetu uliwafanya watembee na kukimbia masafa marefu kwa ajili ya kuwinda au kulima. Wacheze kwenye sherehe. Wabebe mizigo wakati wa kilimo au mavuno.
Siku hizi mtindo wetu wa maisha ni tofauti. Tunakaa zaidi maofisini; viti vya starehe vimekuwa marafiki wetu wakubwa. Tunasafiri kwenda kazini kwa magari, pikipiki na mabasi. Baada ya kazi, tunapumzika kwenye sofa tukitazama televisheni kabla ya kwenda kulala.
Mara chache sana tunajihusisha na shughuli zinazotulazimisha kutembea au kusogea mara kwa mara, isipokuwa kama kazi yetu ni ya nguvu. Mtindo huu wa maisha husababisha matatizo mengi, kama mkao mbaya wa mwili, uzito kupita kiasi, mzunguko duni wa damu, na hatari kubwa ya magonjwa.
Kisha mtu akaamua kutatua tatizo letu kwa njia ya mkato: gym. Sasa tunaiona gym kama njia yetu kuu ya kubaki active. Gym ni nzuri, lakini inatangazwa kana kwamba mazoezi pekee ni kunyanyua vyuma au cardio.
Njia hii huvutia zaidi kwa sababu matokeo yake ni rahisi kuyaona. Kwa mfano, nilipoingia gym kwa mara ya kwanza mwaka 2011, mwaka wangu wa kwanza katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, niliona jambo hili moja kwa moja.
Nilifika huko peku na nimevaa jezi ya mpira, nikiwa na rafiki yangu mkubwa Jabir. Tulionekana hatupo sehemu sahihi kabisa. Tuliona wanaume wenye mikono mikubwa, vifua vilivyojaa, na miguu ya aina ile unayoiona tu kwenye filamu.
Tuliona wanawake wazuri wamevaa kaptula fupi sana. Walivaa sidiria za kubana zilizo tufanya tujiulize kama kweli tuliruhusiwa kuwaangalia hadharani.
Baada ya miaka mingi ya kwenda gym, naweza kufupisha siri ya kufanya mazoezi. Ni rahisi: tafuta njia ya kuusogeza na kuupa kazi mwili wako, kama vile bibi yangu alivyofanya.
Mwili unakuwa na nguvu, imara na bora unapofanya kazi. Kama hujawahi kutembea kilomita chache maishani mwako, basi anza kwa kutembea hadi uchoke. Kesho yake ongeza umbali kidogo. Fanya hivyo hadi umbali huo uanze kuhisi mwepesi.
Kisha jisukume zaidi. Anza kwa kutembea kwenye vilima au milima. Halafu ongeza uzito unaobeba au tembea kwa kasi zaidi ili kuongeza ugumu.
Unaweza kufanya hivyo popote. Hauhitaji gym ili kufanikisha hilo. Mababu zetu hawakuwa na gym, dunia ndiyo ilikuwa gym yao. Kazi za nguvu kama ujenzi na kilimo mara nyingi hutatua tatizo hilo.
Kama unafanya kazi ofisini, tafuta namna ya kufanya mwili wake usogee au ufanye kazi katika siku yako. Anza kwa kutembea, kisha ongeza kiwango cha ugumu. Inapohisi rahisi, jaribu kukimbia au kubeba uzito wa ziada ili kuendelea kujipa changamoto.
Sehemu nyingine ya jinsi ya kujenga na kutunza mwili ni kunyoosha misuli na viungo tofauti vya mwili. Kama uko kwenye miaka yako ya thelathini au zaidi, unaweza kugundua kwamba baadhi ya harakati zinaanza kuwa ngumu zaidi. Unaona kwamba inakuwa vigumu zaidi kuinama au kupiga magoti.
Labda umeona kugusa vidole vya miguu kumekuwa jambo lisilowezekana. Au ukikaa chini na kunyoosha miguu, hauwezi kuinama kuifikia. Kila sehemu inauma, kama vile umegongwa na treni—shingo, mgongo, mabega, na mapaja yote yanauma.
Haya yote ni kwa sababu umeacha kunyosha misuli yako. Misuli ni kama mpira wa elastic. Kadiri unavyozinyoosha, ndivyo zinavyokuwa na unyumbufu zaidi. Kadiri usivyozinyoosha, ndivyo zinavyokuwa ngumu zaidi.
Unapoamka, tafuta njia za kunyoosha mwili. Nyosha sehemu zote za mwili wako kwa asili. Piga magoti, tambaa, inama, vuta, sukuma, na tulia. Kadiri unavyonyoosha, ndivyo utakavyokuwa mwepesi na unyumbufu zaidi.
Chakula na vinwaji ndio nishati ya mwili
Ili mwili usogee na kufanya kazi vizuri, unahitaji nishati. Kile tunachokula na kunywa kinaamua ubora wa nishati tunayoingiza mwilini. Nishati nzuri inaongeza ufanisi wa mwili kwenye kufanya kazi yake. Nishati mbovu huathiri ufanyaji kazi wa mwili na huishia kuharibu mwili.
Sehemu kubwa ya lishe ya bibi yangu ilitoka shambani kwake. Alikuwa na unga wa mahindi, wali, maharage, mboga, mayai, nyama na viungo karibu yake. Alikula lishe ileile ambayo mababu zake walikula.
Na upishi wake ulikuwa rahisi kadiri iwezekanavyo, vitu vingi vilikuwa ni vya kuchemsha. Mara chache sana alitumia mafuta ya kupikia, ambayo sisi ndiyo tulikuwa tunamletea.
Kama una gari, usingeweka mafuta yasiyofaa kutumika. Hauwezi kuweka petroli kwenye gari la diseli ingawa yote ni mafuta. Na kwa hakika usingeweka maji kwenye gari la petroli au diseli.
Vivyo hivyo kwa mwili; haukuumbwa kutumia baadhi ya vyakula na vinywaji ili ufanye kazi vizuri. Hata hivyo, binadamu wamepata njia ya kufanya hivyo, iwe ni kwa ujinga, uraibu, au sababu tusizoweza kueleza.
Binadamu hutumia vitu vinavyouathiri mwili kila siku, kuanzia vyakula vilivyosindikwa viwandani hadi pombe kali na sigara. Na kama gari ambalo lingeharibika baadaye baada ya kujazwa mafuta yasiyofaa, mwili nao hujibu kwa namna hiyo.
Magonjwa yasiyo ya kuambukiza ni matokeo ya kuutumia vibaya mwili. Shinikizo la damu kutokana na pombe nyingi na nyama nyingi, au saratani kutokana na uvutaji sigara, vinaonyesha jinsi mwili unavyojibu mazoea mabaya.
Mababu zetu walikuwa na lishe rahisi, wakila na kunywa vitu walivyovikuta kwenye mazingira ya asili au walivyolima, kufuga na kuwinda.
Ukienda dukani au mgahawani, jiulize: bibi yako angefikiria nini kuhusu chakula ulichonunua au ulichoagiza?
Upe mwili wako nishati sahihi na utakutumikia vizuri. Kama tayari unatumia mara kwa mara vyakula na vinywaji visivyo na afya, jitahidi kuvipunguza na kutumia kwa kiasi.
Namna tunavyopumzika huathiri namna tunavyofanya kazi
Kwa miaka yote ambayo nimemfahamu bibi yangu, hakupenda sisi kukaa kwake hadi usiku sana. Alitaka kulala mapema na kuamka mapema. Alisema Mungu wake anatumia jua kama mwongozo wa maisha yake.
Jua linapotoka, yeye anaamka; jua linapozama, yeye analala. Kisayansi, kuna ushahidi kwamba miili yetu hufanya kazi kwa kuzingatia mizunguko ya asili ya mwili, yaani circadian rhythms. Tunafanya kazi vizuri zaidi tunapoamka na jua na kupumzika linapozama.
Kama unaweza, jitahidi kuifuata asili. Amka mapema, anza siku yako. Punguza shughuli jua linapozama na nenda kulala. Huo ndio usingizi wa asili ambao mwili wako unahitaji.
Ndiyo, unaweza kuendesha gari kwa umbali mrefu sana, usiku na mchana bila kupumzisha wala kufanya service; lakini kwa gharama gani? Na kwa muda gani?
Miili yetu hufanya kazi kwa namna hiyo hiyo; unaweza kuisukuma kwa siku, wiki, au hata miezi. Lakini mwishowe, uchovu utakufikia na utaharibika. Na gharama hiyo ni kubwa sana kuilipa. Unaweza kutengeneza na kubadilisha gari, lakini hauwezi kufanya hivyo kwa mwili wako.
Tafuta njia za kuupumzisha mwili wako. Lala unapoweza, angalau saa saba hadi nane. Pumzika katikati ya shughuli zenye nguvu nyingi. Chukua likizo kidogo baada ya kumaliza miradi mirefu au kazi inayochosha.
Bibi yangu alikuwa analala mapema ili kuhakikisha ana nguvu za kutosha kwa siku inayofuata. Wakati si msimu wa kupanda au kuvuna, kazi zake za mwili hupungua. Hilo husaidia mwili wake kupumzika na kupona.
Kwa muhtasari, miili yetu inahitaji kutembea, kufanya kazi na kunyoshwa viungo, kupata virutubisho, na mapumziko ili ifanye kazi vizuri kwa muda mrefu iwezekanavyo. Ukiyazingatia hayo, hautahangaika sana kuhusu kutokuwa fiti, kuwa mnene kupita kiasi, au kupata magonjwa yanayozuilika.
Akili
Mwili ni chombo kinachobeba uhai na maisha yetu; akili ndiyo namna tunavyoutafsiri uhai na maisha.
Kuna hadithi maarufu sana kuhusu mapacha waliokulia na baba mlevi. Walipokua, walichagua njia tofauti. Pacha wa kwanza akawa mlevi. Alipoulizwa kwa nini, akasema, “Baba yangu alikuwa mlevi, ulitegemea niwaje sasa?”
Pacha wa pili alipokuwa akawa anachukia pombe. Alipoulizwa kwa nini, akajibu, “Kwa sababu baba yangu alikuwa mlevi. Sikupenda namna alivyokuwa anaishi, alivyotutesa, na jinsi alivyoharibu maisha yake. Sikupenda kuwa kama yeye.”
Mapacha wawili waliofanana kila kitu na kuishi nyumba moja chini ya baba moja, lakini walikuwa na mtazamo tofauti. Hivyo ndivyo akili inavyofanya kazi. Inaunda namna tunavyoiona dunia, tunavyotafsiri matukio, na tunavyotengeneza uhalisia wetu wenyewe.
Nilisikia hadithi kuhusu nyumba ya kwanza ya bibi yangu kuungua. Moto uliharibu kila kitu alichokuwa amekijenga kwa miaka mingi sana.
Watoto wake walipompa wazo la kumsaidia kuhamia mjini aanze maisha mapya, alisema, “Nitajenga nyumba mpya, nitaanzisha mashamba mapya, na nitapanda mazao yangu tena. Niliweza mara ya kwanza; nitaweza tena.”
Na kweli, alifanya hivyo. Hadi siku aliyokufa, aliendelea kuishi kwenye ardhi yake. Na walimzika kwenye ardhi hiyo hiyo. Huo ndio ulikuwa mtazamo wake wa maisha.
Mambo matatu muhimu kuhusu akili ni: uwazi wa kuona mambo, nidhamu, na utulivu wa akili.
Uwazi
Uwazi ni uwezo wa kuona mambo kama yalivyo na kuyakubali. Kama nilivyosema hapo awali, watu tofauti wanaweza kutafsiri hali ileile kwa namna tofauti. Mtu mmoja anaweza kuona sita, mwingine akaona tisa, kutegemea upande aliosimama na wote wakawa sahihi.
Jiweke katika mazingira yatakayokusaidia kuona mambo kwa uwazi. Hivyo utaimarisha mtazamo wako na kufanya maamuzi bora zaidi.
Mazingira tofauti na mitazamo tofauti hujenga uwazi.
Jijengee tabia ya kukutana na watu wapya, kutembelea sehemu tofauti, na kutafuta vyanzo mbalimbali vya taarifa na ujuzi kama vitabu. Tabia hizi zitakupa zana za kujenga uwazi wa akili.
Nidhamu
Akili ni kitu chenye ujanja; inaweza kuwa bosi wako au mtumishi wako kutegemea na namna unavyoitumia. Usipofanya chochote kwa makusudi, akili itakuja na mawazo ya ajabu sana.
Ipe akili yako nidhamu mara kwa mara, na unaweza kufikia malengo yako. Pia utafurahia maisha kwa namna za kuvutia. Watu wanaweza hata kukuita genius.
Unahitaji kuifundisha akili yako ifikiri nini, ifikiri lini, na ichakataje taarifa. Unahitaji kuitawala mifumo yako ya mawazo.
Ukiiacha iende ovyo, matatizo yatakufuata. Hii ni pamoja na uraibu, uvivu, wasiwasi, na hofu. Matatizo mengi ya maisha hutokana na ukosefu wa nidhamu.
Kila tatizo linalosababishwa na ukosefu wa nidhamu hutokana na kushindwa kuitawala akili.
Utulivu wa akili
Umeshawahi kusikia msemo unaosema, “unahitaji akili iliyotulia maishani.”
Ukosefu wa uwezo wa kuona mambo kama yalivyo na nidhamu huwa unasababisha vurugu ndani ya akili. Hii hufanya kuishi maisha ya shida sana.
Baadhi ya watu wanapata shida kupata amani katika mahusiano yao. Huenda wanakosa uwezo wa kuona mambo kwa usahihi katika kuchagua wapenzi sahihi. Pia wanahitaji nidhamu ili kujenga na kudumisha mahusiano yenye afya.
Wengine wanakosa amani ya akili katika kazi na taaluma zao. Mara nyingi hili hutokea kwa sababu hawakupata mwongozo wa wazi walipochagua kazi, biashara, au shughuli walizotumia miaka mingi ndani yake. Pia wanakosa nidhamu ya kubadili mwelekeo wa maisha yao ya kikazi.
Amani ya akili ni matokeo ya uwezo wa kuona mambo kama yalivyo na nidhamu; jitahidi kujenga yote mawili na utavuna utulivu huo.
Cha kusikitisha, hakuna mtu anayeweza kukuletea utulivu wa akili. Lazima uijenge mwenyewe.
Matatizo mengi ya binadamu hutoka akilini. Ukosefu wa uwezo wa kuona vitu kama vilivyo na kwa uwazi na nidhamu siku zote utaishia katika ukosefu wa amani ya akili. Jifunze kuyafanyia kazi hayo na utaongeza zana muhimu sana katika maisha yako.
Mtazamo wako wa akili unaamua namna unavyoona maisha. Ili upate amani ya akili, unahitaji uwezo wa kuona vitu kama vilivyo na nidhamu. Hivyo ndivyo utakavyoweza kutafsiri maisha kwa namna inayokufaa.
Nafsi/Roho
Hii ni mada ambayo kwa watu wengi ni kama mwiko fulani. Kutokana na ujinga, udanganyifu, na kutokuwa na uhakika, watu wengi wanahangaika na masuala ya kiroho.
Bibi yangu aliposema, “Mimi ni binti mpendwa zaidi wa Mungu,” nilihisi viongozi wa kanisa walikuwa wamemshawishi. Ilionekana kama anaamini kila kitu maishani kinazunguka kwa Mungu. Nina marafiki na ndugu wengi wanaofanya mada ya Mungu ionekane ya kuudhi au ya kutia mashaka.
Sasa natambua kwamba bibi yangu alikuwa akizungumzia sehemu ya kiroho ya afya yake.
Utafiti wangu ulinionyesha mambo matatu muhimu: maana ya maisha, kuishi kwa kulingana na maana hiyo, na kuamini katika kitu kikubwa kuliko wewe mwenyewe.
Maana
Maisha yanaweza kumaanisha chochote kwa mtu yeyote; na hilo ndilo linaloyafanya yawe magumu. Maana ya maisha ya bibi yangu na yangu ni kama mchana na usiku. Maana yangu ni tofauti na yako. Na hilo ndilo pia linaloyafanya yawe na maana.
Katika harakati yangu ya kuelewa maana ya maisha, nilijifunza kusimama na kujiuliza maswali haya:
Kwa nini nipo hai duniani?
Maisha yangu ni kwa ajili ya nini?
Ni nini kinachofanya mateso yawe na thamani ya kuvumiliwa?
Ni kitu gani kinachostahili kuyatoa maisha yangu kwa ajili yake?
Niligundua maana ya maisha kwangu ni mimi kuwa bora kwanza. Kuwa binadamu bora, mtoto bora, rafiki bora, jirani bora na mfanyabiashara bora. Nikiwa bora nitakuwa na nyenzo na uwezo wa kuwasaidia wengine kuwa bora zaidi katika muda huu mfupi tulio nao hapa duniani. Maisha yangu ni ya kutumikia, na yanastahili mateso yote yanayohitajika ili kufanya hivyo.
Kusikia ndugu, mwanafamilia, rafiki, au hata mtu baki akisema kwamba nilibadilisha maisha yake kuwa bora kunaniletea furaha kubwa sana. Kujua hilo kunafanya juhudi zangu zote ziwe na thamani.
Ninapenda simulizi na hadithi zenye mafunzo ya maisha tangu darasa la tatu katika Shule ya Msingi St Joseph. Sijawahi kuacha kutafuta maarifa na kuyatumia katika maisha yangu. Pia sijawahi kuacha kusimulia watu au kuweka sehemu yeyote ambayo wengine watayapata pia.
Nitatoa msaada wa maarifa kupitia mazungumzo ya mtu mmoja mmojo tukikutana, kwenye simu, au kupitia mtandao. Nitafanya hivyo kwa kuandika picha, video, sauti, au njia yoyote mpya inayojitokeza.
Sikuacha kufanya hivyo nilipokuwa shule ya msingi, sekondari, chuo kikuu, au nilipokuwa nafanya kazi PwC. Sikuacha nilipoanzisha biashar yangu ya kwanza, na sijaacha sasa nikiwa mjasiriamali mwenye uzoefu.
Hiyo ndiyo dhamira yangu. Hiyo ndiyo inayoyapa maisha yangu maana: kuwa bora zaidi na kuwasaidia wengine kufanya hivyo kupitia hadithi na mawazo yanayochochea fikra na kukua. Yako ni ipi?
Kaa chini na jibu maswali haya ya muhimu zaidi:
Kwa nini upo hai duniani?
Maisha yako ni ya nini?
Ni nini kinachofanya mateso yawe na thamani ya kuvumiliwa?
Ni kitu gani kinachostahili kuyatoa maisha yako kwa ajili yake?
Usipoyajibu maswali hayo, siku zote utahisi kuna kitu kinakosekana, bila kujali unafanikisha nini. Unaweza kuwa na pesa zote duniani, familia na marafiki bora kabisa, lakini unapolala usiku utahisi upweke wa ndani.
Umetumia miaka mingi kuingia katika tafsiri za wengine kuhusu maana ya maisha. Mtu alikuambia nenda shule, pata kazi, fanya kazi hadi ustaafu, kisha ufe. Je, hicho ndio kitu pekee kwenye maisha yako?
Huenda umesikia kuhusu fursa ya biashara inayoahidi pesa nyingi. Ukaanzisha na ikaleta faida, utajuaje wakati umefika kusema unayo faida ya kutosha? Na utafanya nini na utajiri huo?
Inawezekana kuna mtu alisema unapaswa kuwa kiongozi na kukusanya nguvu na mamlaka, na ukafanya hivyo. Lakini utajuaje lini inatosha? Na utafanya nini mamlaka yatakapobadilisha mikono?
Kile ulicho nacho, unachofanya, unaowajua, na ulipo haviwezi kufafanua maana ya maisha yako. Kaa chini na jibu maswali haya ya muhimu zaidi:
Kwa nini upo hai duniani?
Maisha yako ni ya nini?
Ni nini kinachofanya mateso yawe na thamani ya kuvumiliwa?
Ni kitu gani kinachostahili kuyatoa maisha yako kwa ajili yake?
Ukishayapata majibu hayo, utaanza haraka kupanga unachofanya, unafanya na nani, na unafanya vipi. Maisha peke yake hayana maana. Utalazimika kutafuta maana yako mwenyewe na kuipa maisha. Usipofanya hivyo, mtu mwingine atakupangia maana yake.
Kuishi kulingana na maana ya maisha yako
Kama kutambua maana ni hatua ya kwanza, basi kuishi maisha yako kwa kufuata maana hiyo ni hatua inayofuata.
Tatizo la kwanza maishani ni kuishi bila kujua maana ya maisha yetu. Tatizo la pili ni kujua maana hiyo lakini kuishi kinyume nayo.
Watu wengi hupata maana ya maisha kwa kuitumikia jamii yao. Hilo linaweza kutokea kupitia biashara, kazi za kijamii, dini, au siasa. Lakini watu wengi wameajiriwa. Hawawezi kuacha kazi kufuata maana hiyo kwa sababu nyingi. Na wanachukia Jumatatu kila wanapoenda kazini.
Wajasiriamali wengi hujenga utajiri kupitia biashara ambazo hawazijali kwa dhati. Kisha baadaye hutoa sehemu kubwa ya pesa hizo kwa mambo wanayoyajali kweli.
Kuishi kinyume na kusudi lako ni kuisaliti roho yako. Katika Biblia Takatifu, Luka sura ya 9 mstari wa 25 inasema: “Itamfaa nini mtu kuupata ulimwengu wote, kisha ajipoteze mwenyewe?” Na katika Qur’an, Surah Al-Baqarah (2:90), inasema: “Ni ubaya ulioje wa bei waliyouza nafsi zao kwayo…”
Mfano maarufu wa kuishi kinyume na kusudi la mtu ni wa Yuda Iskariote. Wengi wanajua simulizi la jinsi Yuda alivyomsaliti Yesu, lakini mara nyingi hatufuatilii kilichotokea baada ya hapo.
Mathayo sura ya 27 mstari wa tatu inasema kwamba “Yuda alipoona Yesu amehukumiwa, alijawa na majuto. Akawarudishia makuhani wakuu na wazee vile vipande thelathini vya fedha. Katika mstari unaofuata, akasema: “Nimetenda dhambi, kwa maana nimesaliti damu isiyo na hatia.”
Baada ya hapo, akaitupa ile fedha hekaluni, akaondoka, kisha akajinyonga (Mathayo 27:5).
Unaweza kufikiria maumivu aliyokuwa nayo Yuda?
Alirudisha fedha, akaonyesha majuto hadharani, halafu akachukua uhai wake mwenyewe.
Maumivu ya nafsi na roho hayawezi kupimika na kuvumilika milele. Haijalishi umepata mafanikio gani mengine duniani, kama nafsi yako haina amani maisha yako yote yatakosa amani.
Kama unachukia kwenda kazini Jumatatu lakini unafurahia Ijumaa, inawezekana kazi yako haiendani na maana na kusudi la maisha yako.
Kama haupendi kutumia muda na mpenzi wako, mke wako, mume wako, au mtu mwingine yeyote, huenda kuna kutokulingana na maana na kusudi la maisha yako na mahusiano yako.
Kama una pesa, magari, majengo, mamlaka, na hadhi lakini bado unahisi utupu, huenda ni kwa sababu matendo yako hayaendani na kusudi na maana ya maisha yako.
Suluhisho ni rahisi: simama na ujiulize:
Kaa chini na jibu maswali haya ya muhimu zaidi:
Kwa nini upo hai duniani?
Maisha yako ni ya nini?
Ni nini kinachofanya mateso yawe na thamani ya kuvumiliwa?
Ni kitu gani kinachostahili kuyatoa maisha yako kwa ajili yake?
Ukishapata majibu hayo, kazi yako ni kuishi kila siku kwa kuzingatia majibu hayo.
Kuishi kwa ajili ya kitu kikubwa kuliko wewe mwenyewe
Bibi yangu aliposema, “Mimi ni binti mpendwa zaidi wa Mungu,” alionyesha ufahamu wa kina kuhusu maisha. Aliamini kuna kitu kikubwa mno kuliko yeye mwenyewe.
Nilimuuliza kuhusu afya yake ya kimwili na mwili wake, lakini jibu lake lilijumuisha kila kitu. Alikubali kwamba kuna kitu kikubwa kuliko yeye, yaani Mungu wake. Na aliamini kwamba, kwa yote aliyopitia, yeye alikuwa binti mpendwa wa Mungu.
Alichagua kuishi maisha yake kwa mtazamo huo. Mtazamo huo uliathiri jinsi alivyotembea, alivyokula na kunywa. Ulimsaidia kupata uwazi, kujenga nidhamu, kugundua maana ya maisha yake, na kuishi kulingana nayo.
Njia bora ya kuyaelewa maisha ni kukubali kwamba kuna kitu kikubwa kuliko wewe kinachofanya kazi katika ulimwengu. Sasa, kwa sababu ya utandawazi na taarifa, mara nyingi tunatumia neno Mungu.
Iwe mtu ni Muislamu, Mkristo, au Mhindu, wazo la uwepo wa Mungu ni la ulimwengu mzima. Hata wale wasio wa dini hutambua kwamba kuna kitu kikubwa na chenye nguvu zaidi katika ulimwengu kuliko binadamu.
Wengine wanakiita mizimu ya mababu, wengine Karma, wengine nguvu asilia, na wengine wanaita sayansi. Kile ambacho wote tunakubaliana nacho ni kwamba sisi binadamu tuna mipaka katika nguvu, ufahamu, ushawishi, na taarifa kuhusu mengi yanayotokea duniani.
Tunahitaji mahali pa kujiegemeza na dira itakayotuelekeza kwenye nchi ya ahadi. Kama dini yako inasema nchi hiyo ni mbinguni, basi sawa. Kama inasema ni mahali panapoitwa Nirvana, bado sawa.
Jiunge na jamii ya watu wanaoshiriki maadili yako, imani zako kuhusu maisha, na imani katika nguvu ya juu. Hilo mara nyingi huleta amani kwa roho. Nenda msikitini na kanisani. Nenda sehemu ya kuabudu.
Baadhi ya watu wenye huzuni zaidi duniani ni wale wanaofanya kila kitu kwa ajili yao wenyewe tu. Wanaishi tu ndani ya vichwa vyao na hawana tumaini wala imani katika kitu kikubwa kuliko wao.
Maisha huwa rahisi zaidi unapokubali kwamba kuna nguvu ya juu inayofanya kazi katika ulimwengu. Mtazamo huo hukusaidia kupata majibu bora zaidi kuhusu kusudi la maisha yako.
Hilo huleta uwezo wa kuona mambo kama yalivyo na nidhamu, na kusaidia akili kubaki thabiti katika kuishi kulingana na kusudi letu. Mtazamo huo hufanya maamuzi kuhusu nini cha kula, kunywa, jinsi ya kusogea, na lini kupumzika kuwa rahisi zaidi. Utakuwa na kusudi la wazi la kukuongoza. Na unahitaji kuwa katika hali yako bora ya kimwili, kiakili, na kiroho ili kufanya hivyo.
Ningependa sana ningekuwa na mazungumzo ya kina zaidi na Anna, bibi yangu, kuhusu afya yake kwa kuzingatia mwili wake, akili yake, na roho yake. Lakini najua angegusa hoja hizi kuu.
Huenda angependekeza nisome haya kwenye mazishi yake. Haya yanabeba somo bora zaidi kuhusu afya na maisha yenye maana. Kwa kuwa hukuwahi kuwa sehemu ya maisha yake, tafadhali ichukulie hii kama wasifu wake wa mazishi.
Unaweza kuwa hauna ugonjwa, lakini hiyo haimaanishi una afya. Mwili uliofiti unaweza bado kuwa na akili yenye vurugu; hiyo si afya. Akili iliyo fiti lakini ndani ya mwili dhoofu na uliochoka si afya. Mwili ulio fiti wenye akili iliyomakini hauna maana kama roho haiko sawa na kusudi lake.
Kumbuka kwamba mwili wako hubeba uhai, akili yako hutafsiri uhai huo, na roho yako huupa maana.
Mpaka wakati mwingine,
Fikiri kwa kina. Ishi kwa makusudi.
Watushule

