Kuna tofauti kati yako na kazi yako.
Kuna kufanya kazi kwa sababu ya pesa, kwa sababu unaipenda au kwasababu unahitaji kukua.
Kuna kipindi katika maisha yangu nilikaa na bibi yangu wa upande wa mama. Katika kipindi hicho, niliishi kwenye nyumba iliyokuwa na zaidi ya watu kumi. Sehemu ya kawaida ya maisha ilikuwa kwenda shambani wakati wa kupanda na kuvuna.
Mwanzoni, nilihisi kama ni kazi ya kulazimishwa. Lakini baadaye nilielewa kuwa hapo ndipo familia ilipopata chakula chake. Babu na bibi yangu walikuwa tayari wamestaafu, na walipaswa kututunza kwa kutupatia chakula wakati tunaishi kwao. Kilimo na ufugaji ndivyo walivyotupatia mahitaji yetu.
Wakati wa likizo, tulilazimika kuamka mapema. Tulitembea umbali mrefu kwenda mashambani na kukaa huko hadi jioni. Kulingana na msimu, tulitumia siku nzima kufanya kazi ngumu.
Baada ya miaka kadhaa, ilianza kuwa ya kufurahisha, kwa sababu majirani wote walifanya hivyo pia. Marafiki wetu walikuwa wanafanya jambo hilohilo. Ikawa sehemu ya maisha. Huo ndio ulikuwa uzoefu wangu wa kwanza wa kazi maishani. Hiyo pia ilikuwa mara ya kwanza kujifunza kwamba nilipaswa kufanya kazi ili kuishi.
Baadaye nilipata uzoefu wangu wa kwanza wa ujasiriamali. Nilikuwa nikimsumbua mama aninunulie viatu vya mpira, na havikudumu kwa muda mrefu. Siku moja aliniambia nifanye kile watoto wa majirani walikuwa wakifanya ili kupata pesa.
Mama yao alikuwa muuzaji wa mboga. Alikuwa anaamka mapema, anakusanya matunda na mboga sokoni , kisha anauza mitaani. Wakati wa wikiendi na likizo alikuwa akiwafundisha watoto wake wafanye hivyo pia. Hivyo ndivyo alivyokimu familia yake, na hivyo ndivyo watoto walivyopata pesa ya matumizi yao binafsi.
Nakumbuka siku yangu ya kwanza. Niliamka mapema nikiwa nimechoka. Nilitembea polepole nyuma ya jirani yetu alipokuwa akinifundisha namna ya kupata mboga na matunda sokoni. Kisha ikafuata safari ndefu ya kurudi nyumbani kuviandaa kwenye beseni la njano.
“Nyunyizia maji mengi kwenye matunda na mboga. Halafu viweke mahali vinapoonekana unapobeba besni kichwani.” Alinielekeza tulipofika nyumbani.
Siku hiyo ya kwanza, nilitembea zaidi kuliko siku yoyote ile kabla yake. Nilikaa masaa zaidi ya matano nikitangaza, “Mboga, matunda, freshi, kutoka sokoni, mpaka mlangoni kwako!” Watoto wa jirani walikuwa wamezoea jambo hilo; hawakutaka kabisa kupumzika. Walisema wanapumzika baada tu ya kumaliza kuuza.
Walimaliza haraka kuliko mimi, na wakachukua mzigo wangu wakauza nao pia. Tukaenda nyumbani; nililala mpaka asubuhi iliyofuata. Huo ndio ulikuwa msukumo wangu wa kwanza wa ujasiriamali.
Wakati wa likizo hiyo, nilirudisha pesa nilizokopa kwa mama, nikaweka akiba ya kununua viatu vyangu vya mpira, na nikajifunza kidogo kuhusu biashara. Huo ulikuwa pia uzoefu wangu wa kwanza wa kufanya kazi kwa ajili ya pesa.
Nilipomaliza mwaka wangu wa pili katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, nilikamilisha mafunzo yangu ya vitendo KPMG Tanzania. Hii ni moja ya kampuni nne kubwa zaidi za ukaguzi wa hesabu duniani. Wakati wa mafunzo yetu, ni watatu tu tulichaguliwa kujiunga.
Huo ulikuwa uzoefu wangu wa kwanza wa mazingira ya kazi ya kitaaluma ambapo ujuzi na muda vilikuwa muhimu kwa ukuaji. Nilijifunza kuhusu sheria na sera za ajira. Nilianza kuelewa utamaduni wa kazi wa saa mbili hadi saa kumi na moja, siasa za ofisini, mishahara, na muhimu zaidi, mzunguko wa watu kuingia na kutoka.
Hapo ndipo nilipoelewa dhana ya kufanya kazi kwa ajili ya kukua, kutoka kuwa intern hadi labda kuwa mkurugenzi au hata partner siku moja.
Wakati wa mafunzo yangu KPMG, nilijifunza namna kampuni zinavyosajiliwa, zinavyopata pesa, na zinavyokua. Hii ilinipa mtazamo wa juu zaidi kuhusu biashara kuliko ule niliopata kwa kuuza matunda na mboga barabarani.
Uzoefu huo ulinipa hamasa ya kuanzisha kampuni yangu ya kwanza, AweDin, ambayo ilikuwa ni kifupi cha Awesome Dinero
Kampuni hiyo ya kwanza nikiwa chuo kikuu ilikuwa msingi wa biashara nyingi za baadaye. Biashara moja ilipelekea nyingine kwa miaka mingi, na inaendelea hadi leo. Hizi zilijumuisha AweSome Magazine, MobiAd, Emakat, Watushule, na sasa Mentamo.
Katika hatua zote hizi za maisha, kuna jambo moja ambalo halijawahi kubadilika. Daima nimeendelea kulipa kipaumbele bila kujali nini kilikuwa kinaendelea maishani mwangu. Hicho ni usimulizi wa hadithi.
Kitabu cha kwanza cha hadithi nilichosoma kilikuwa darasa la tatu, kitabu alicholeta mama nyumbani kuanzisha maktaba yetu ya kwanza ya nyumbani.
Kilikuwa kitabu rahisi kuhusu vyura na sungura, na mafunzo wanayoleta maishani. Nilipenda mtindo wake na nguvu ya hadithi kufundisha. Nilianza kutafuta vitabu zaidi, nikajiunga na maktaba ya taifa. Nilianza kuhudhuria vilabu vya vitabu na matukio ya kifasihi.
Kadiri nilivyojifunza zaidi, ndivyo nilivyotaka zaidi kushirikisha maarifa yangu. Nilianza kuandika kuhusu mafunzo hayo. Nilijiunga na midahalo shuleni na kutoa hotuba za Jumatatu asubuhi katika shule ya msingi St Joseph na shule ya sekondari Pugu.
Nilianza kushirikisha hayo mtandaoni kwa namna yoyote iliyokuwa rahisi—machapisho, sauti, video, au makala. Na sasa tupo hapa; ama unasoma haya mahali fulani au unayasikiliza au unayatazama. Niligundua shauku yangu katika usimulizi wa hadithi bila malipo wala kuchoka; nilifanya kazi hiyo kwa sababu tu niliipenda.
Safari yangu inaweza kuonekana ya kipekee kwa namna yake. Lakini ukiangalia sababu ya ndani, inaakisi ukweli wa jumla kuhusu namna tunavyoishi. Watu hufanya kazi ili kuishi, kufanya kazi ili kukua, au kufanya kazi kwa ajili ya shauku zao na vitu wanavyopenda.
Kazi imebadilika kwa vizazi vingi. Sasa tunaishi katika zama za AI, lakini baadhi ya mambo yanafanana na enzi za wawindaji na wakusanyaji. Hizo zilikuwa zama ambazo binadamu hawakuwa na makazi ya kudumu.
Mwanzoni, binadamu walifanya kazi ili kuishi tu. Wanakikundi waliokuwa na afya na nguvu walikuwa wanawinda na kukusanya chakula. Wengine walikuwa wanalinda na kuwahudumia watoto na wagonjwa.
Kisha zikaja zama za kilimo. Hapo ndipo maisha yalibadilika kwa jamii hizo. Jamii zilianza kuwa na mashamba na kufuga mifugo. Hii ilimaanisha walianza kukaa eneo moja kwa muda mrefu zaidi.
Katika kipindi hicho, kazi ilipanuka. Baadhi ya watu wakawa wakulima tu, wengine wakawa wafugaji. Na hapo ndipo tabaka katika jamii zilianza kujitokeza, wamiliki na wafanyakazi. Pia ilileta dhana ya ziada ya mazao, kwa sababu watu waliweza kuhifadhi mavuno yao. Hapo ndipo pia dhana ya hadhi ilipoanza kujitokeza.
Watu waliwaona wenye mashamba makubwa, mifugo mingi, wafanyakazi wengi, na akiba ya mazao kama matajiri. Matajiri waliheshimiwa zaidi katika jamii na walipata nguvu.
Kilimo kiliendeleza zama za ustaarabu, ujuzi, na ufundi. Hii ilisababisha ubunifu na ukuaji hadi pale mapinduzi ya viwanda yalipojitokeza. Hili lilikuwa badiliko jingine katika historia ya binadamu; sasa watu walikuwa wanaenda kufanya kazi viwandani na kwenye mitambo.
Aina nyingi za nafasi zilijitokeza. Hizi zilijumuisha vibarua, waendesha mashine, na wafanyakazi wa viwandani. Pia kulikuwa na wahasibu, makarani, na mameneja. Enzi hii ilileta uchumi wa kisasa na kuanzishwa kwa ofisi.
Maisha ya kisasa ya mijini yalimaanisha kwamba watu wazima waliondoka kwenda kazini asubuhi. Walitumia siku zao ofisini, wakiuza muda wao na ujuzi wao hadi jioni. Walifanya hivyo kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa na baadhi ya Jumamosi. Mazingira haya yalisaidia kujenga taaluma za mabenki, madaktari, walimu, na wanasheria.
Shule ziliunda programu za kuwaandaa watoto kufuata mzunguko huohuo. Hii iliweka njia iliyo wazi: kwenda shule, kufaulu mitihani, kuingia chuo kikuu, na kufanya kazi hadi kustaafu. Mzunguko huu uliendelea kwa miaka mingi hadi intaneti ilipowasili.
Intaneti iliondoa vikwazo vingi kuhusu wapi, lini, na na nani watu wanafanya kazi. Iliondoa dhana kwamba mtu lazima afanye kazi ofisini pekee. Pia iliwezesha watu kufanya kazi pamoja kutoka popote duniani.
Intaneti iliongeza utandawazi na usambazaji wa taarifa. Iliunda nafasi mpya za ajira na majukwaa ya watu kuuza muda wao, ujuzi wao, na utaalamu wao.
Taaluma mpya zilijitokeza, zikiwemo freelancers, consultants, traders, YouTubers, influencers, na wachekeshaji.
Na sasa tunaingia katika zama za AI. Bado hatujui kiwango ambacho hili litabadilisha mazingira ya kazi. Lakini kwa ishara za sasa, tunaona kwamba AI itachukua sehemu kubwa ya kazi zilizojengwa katika enzi zilizopita.
Mashine zitachukua sehemu kubwa ya kazi za mikono kutoka enzi za kilimo na viwanda. Roboti zitachukua sehemu kubwa ya kazi za ofisini zinazohitaji marudio na uthabiti.
Mifumo ya AI kama ChatGPT na Claude itachukua kazi nyingi zinazotegemea ujuzi katika maeneo kama uhasibu, sheria, upigaji picha, sanaa, na uandishi.
Tunaelekea katika zama ambapo mali yenye thamani kubwa zaidi sokoni ni kuwa binadamu. AI haiwezi kuiga uzoefu, hisia, mahusiano ya kibinadamu, ndoto, na malengo.
Lakini hilo halibadilishi ukweli wa kwa nini watu wanafanya kazi. Kazi hubadilika kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Sasa, tunapaswa kuikabili vipi kama mtu binafsi? Suala si kuwa umeajiriwa au umejiajiri.
Tatizo ni kwamba kazi, iwe ya ajira au ya kujiajiri, imekuwa utambulisho wetu. Wengi wetu tunafikiri kazi yetu ni mwendelezo wa sisi wenyewe. Hilo husababisha matatizo mengi katika maisha yetu. Wengine huendelea kufanya kazi mbaya kwa sababu wanafikiri hawawezi kubadili taaluma.
Watu wengine hubaki kwenye biashara zinazoshindwa kwa sababu utambulisho wao umeunganishwa nazo. Wengine hufuatilia shauku na vitu wanavyopenda zisizolipa kwa sababu mambo hayo ndiyo yanayowaeleza wao ni nani au walipaswa kuwa nani.
Mambo muhimu zaidi maishani huja kwa tatu, na hivyo ndivyo ilivyo pia kwa kazi.
Kazi, iwe umeajiriwa au umejiajiri, inafanywa kwa sbabu ya pesa, shauku (kupenda), au ukuaji. Hatua tofauti za maisha zinahitaji madhumuni tofauti ya kazi.
Kuna wakati unapaswa kufanya kazi kwa ajili ya pesa, ili kuishi.
Kuna wakati unapaswa kufanya kazi kwa ajili ya shauku, ili kustawi.
Kuna wakati unapaswa kufanya kazi kwa ajili ya ukuaji, ili kuimarika.
Kufanya kazi kwa ajili ya pesa
Kufanya kazi kwa ajili ya pesa ndiyo sababu ya kiuhalisia zaidi. Sikuweza kubishana na bibi yangu kuhusu kupanda au kuvuna nilipokuwa chini ya paa lake. Chakula tulichopata mashambani ndicho tulichokula.
Tulikiuza baadhi yake kwa majirani na marafiki ili tupate vitu vingine vilivyohitajika kwa maisha yetu, kama sukari, mafuta ya kupikia, nguo, na mengineyo.
Nisingeweza kukataa wazo la mama yangu la kuuza matunda na mboga. Kwa njia hiyo, ningeweza kupata pesa za kununua viatu vyangu vya mpira. Hitaji hilo lilikuwa muhimu sana kwangu kiasi kwamba nilikuwa tayari kufanya kazi ili kupata pesa hizo.
Pesa huleta uhai, utulivu, heshima, chaguzi, na wajibu. Hulipa kodi. Huihudumia familia. Hutoa uhuru wa kujitegemea. Hakuna jambo la juu juu katika kutaka pesa. Mara nyingi kutafuta pesa si tamaa. Ni usalama. Ni nafuu ya maisha. Ni uwezo wa kusimama kwa miguu yako mwenyewe na kuwasaidia wengine.
Lakini pesa zina mipaka.
Pesa zikiwa ndio sababu pekee ya kufanya kazi, mtu anaweza kujisikia mtupu ndani hata kama anaonekana amefanikiwa nje. Anaweza kupata pesa vizuri, lakini asipate maana. Anaweza kuishi kitajiri, lakini akafa kihisia polepole. Kazi inapokuwa muamala tu, roho huanza kujitenga na kile ambacho mwili unafanya kila siku.
Kwa hiyo pesa ni muhimu, lakini haitoshi.
Kufanya kazi kwa ajili ya shauku au kupenda kitu
Kufanya kazi kwa ajili ya shauku au vitu unavyopenda kunaonekana kuwa jambo la heshima. Nimekuwa nikipenda daima namna hadithi zinavyogusa maisha ya watu kwa kina, mara nyingi zikibadilisha vizazi kwa ubaya au kwa wema. Yesu na Muhammad, kwa mfano, wamegusa maisha ya mabilioni ya watu kupitia hadithi kuhusu Mungu.
Mababu na mabibi walishirikisha maono yao, matumaini yao, hofu zao, na ndoto zao kwa jamii kupitia hadithi. Hadithi tunazosikia na tunazojiambia ndizo zinazounda maisha yetu. Nimetumia sehemu kubwa ya maisha yangu ya utu uzima kutafuta hadithi na kuzishirikisha.
Shauku au kufanya kitu unachopenda huleta nguvu, uhai, udadisi, ubunifu, na maana. Unapojali jambo kwa kina na kulipenda, kazi huwa nyepesi zaidi. Unaweza kuvumilia changamoto nyingi zaidi pale kazi inapohusiana na maisha yako ya ndani. Shauku na kufanya unachopenda hufanya jitihada ziwe za hiari badala ya kulazimishwa.
Lakini shauku na kufanya unachopenda nayo ina mipaka. Mara nyingi niliacha kutafuta au kushirikisha hadithi kwa sababu mchakato ulikuwa mgumu mno. Wazo la Watushule lilinijia nilipokuwa mwanafunzi wa Kidato cha Nne katika Shule ya Sekondari Pugu. Hiyo ilikuwa mwaka 2008. Nimekuwa nikiingia na kutoka kwenye wazo hili kwa zaidi ya miaka 16.
Shauku na kitu unachokipenda inaweza kubadilika badilika. Hutahisi msukumo kila siku. Baadhi ya kazi zenye maana kubwa bado huwa na urudiaji, kuchosha, usimamizi wa kawaida, marudio, na kujitoa mhanga.
Pia, si kila shauku au kitu unachokipenda kinaweza kulipa bili mara moja. Kuweka matumaini yote kwenye shauku au kitu unachokipenda pekee kunaweza kuleta changamoto za kifedha, kukosa nidhamu, au kukatishwa tamaa na uhalisia wa maisha.
Kufanya kitu unachopenda na shauku ina nguvu, lakini si ya kutegemewa kila wakati.
Kufanya kazi kwa ajili ya ukuaji
Huu ni mtazamo wa muda mrefu. Nilipoanza kama intern KPMG, sikujua chochote kuhusu ulimwengu wa ukaguzi wa hesabu na fedha. Sikujua chochote kuhusu nafasi za ngazi ya ushirika. Nilijifunza kwamba nikifanya kazi vizuri kwa muda mrefu, nilikuwa na nafasi ya kuwa mkurugenzi au hata partner.
Kwa kusoma aina mbalimbali za ukaguzi na namna kampuni zinavyofanya kazi, nilipata uelewa wa kina zaidi wa mifumo ya biashara pamoja na fedha binafsi na za mashirika.
Ilikuwa rahisi kwangu kuhamia PwC, kampuni nyingine miongoni mwa kampuni kubwa nne za ukaguzi duniani. Na niliona njia wazi kutoka kuwa associate hadi kuwa mkurugenzi. Nilijifunza zaidi kuhusu namna ulimwengu wa biashara unavyofanya kazi.
Nilijifunza siasa za ofisini, utamaduni wa saa mbili hadi saa kumi na moja, hustle culture, na kila kilicho katikati yake. Niliweza kuonja ajira huku nikiendesha kampuni yangu changa mwenyewe. Nilijifunza dhana ya nyenzo na namna watu wanavyopata pesa kwa njia tofauti.
Nilijifunza namna ukuaji wa kampuni na biashara ungeunda mtu nitakayekuwa baadaye, na nilijua kutakuja wakati ambao ningepaswa kufanya uchaguzi.
Hii ina maana ya kuchagua kazi si kwa ajili ya pesa au raha ya sasa tu, bali kwa ajili ya mtu ambaye inakusaidia kuwa. Kazi inayolenga ukuaji hujenga ujuzi, tabia, nidhamu, ustahimilivu, uamuzi mzuri, subira, na umahiri. Wakati mwingine kazi unayoihitaji zaidi siyo kazi unayoipenda zaidi leo, bali ni kazi inayokuandaa kwa ajili ya kesho.
Ukuaji unaweza kuhalalisha mapambano.
Kazi ngumu inaweza kuwa ya thamani kwa sababu inajenga akili yako. Kipindi cha hadhi ya chini kinaweza kustahili kuvumiliwa kwa sababu kinajenga msingi wako. Fursa isiyo kamilifu bado inaweza kuwa na thamani kwa sababu inapanua uwezo wako.
Lakini ukuaji nao una mipaka.
Mtu akiishi daima kwa ajili ya ukuaji wa baadaye, anaweza asifurahie maisha yake ya sasa hivi. Maisha yanageuka kuwa maandalizi ya kudumu. Anaendelea kujisukuma, kuchelewesha, kujiboresha, na kuacha vitu. Ukuaji unaweza kuwa mtego mwingine ikiwa unageuka kuwa kujiboresha kusikoisha bila amani.
Kwa hiyo kila sababu ya kufanya kazi ina mazuri yake, na kila sababu ina hatari yake.
Pesa bila maana hugeuka kuwa mateso. Shauku na kufanya kazi unayopenda bila malipo ni mateso. Kufanya kazi unayokua na yenye pesa bila malipo na bila mapunziko nayo ni mateso.
Hiyo ndiyo changamoto ya kazi.
Mtu mwenye hekima huanza kuelewa kwamba swali la kweli si, “Nitachagua lipi milele?”
Swali la kweli ni: Ni kipi kinapaswa kuongoza katika msimu huu wa maisha yangu?
Misimu tofauti inahitaji vipaumbele tofauti.
Katika hatua moja, pesa zinaweza kuhitaji kuongoza. Ikiwa unapambana, una msongo wa mawazo, unalea watoto, au unajaribu tu kuendelea kuishi, huenda usiwe na nafasi ya kuzingatia kile unachokipenda. Katika msimu huu kufanya kazi kwa ajili ya pesa si usaliti. Ni hekima.
Katika hatua nyingine, ukuaji unaweza kuhitaji kuwa kipaumbele. Unaweza kukubali usumbufu, malipo madogo, au kutambuliwa kwa kuchelewa. Hii ni kwa sababu unajenga ujuzi ambao utakuwa wa thamani baadaye.
Katika hatua nyingine, shauku na kufanya kitu unachopenda inaweza kuhitaji kuongoza. Mara baada ya kuwa umetulia na kuwa na ujuzi unaofaa, unaweza kutaka kusogea kwenye kazi inayolingana kwa kina na wewe ni nani.
Tatizo huja pale watu wanapotumia kipimo kisichofaa kwa msimu usiofaa.
Katika msimu wa kutafuta pesa, mtu anajisikia hatia kwa kutofuatilia “shauku yake au kufanya kitu anachopenda.” Mtu aliye katika msimu wa kujifunza anakosa subira kwa sababu ukuaji bado haulipi. Mtu aliye katika msimu wa kustawi anaendelea kukimbiza pesa huku akipuuza kazi anayoijali kwa kweli.
Mvutano upo kati ya pesa, shauku/unachopenda, na ukuaji.
Pia upo kati ya mahitaji ya sasa, uwezo wa baadaye, na wito wetu wa ndani.
Siku zote nimemtazama baba yangu kama hamasa na funzo kubwa la maisha. Alianza kazi yake ya kwanza benki mara tu baada ya kumaliza chuo kikuu. Kazi yake ilimpa kipato chake cha kwanza thabiti na mazingira ya kazi ya kukua sana.
Katika kilele cha kazi yake, alikuwa mkuu wa huduma kwa wateja katika mojawapo ya benki kubwa za kimataifa nchini. Wasifu wake wa mtandao wa LinkedIn ulisema:
“Nimekuwa katika sekta ya benki kwa miaka 29. Nilianza kama msaidizi daraja la kwanza na nikapanda hadi ngazi ya usimamizi. Dhamira yangu ni kuendesha taasisi yangu mwenyewe na kusaidia jamii yangu.”
Baba yangu alifariki kabla hajatimiza dhamira hiyo.
Miezi michache kabla ya kufariki, alikuwa amemaliza kusajili kampuni yake. Alikusudia kutoa huduma za kifedha na kusaidia jamii yake. Lakini hakupata nafasi ya kuiendesha kama alivyokuwa amepanga.
Mara nyingi hujiuliza baba yangu alikuwa anawaza nini alipoamua kustaafu, kuanzisha kampuni yake mwenyewe, na kufuatilia shauku yake ya kusaidia jamii. Ninawaza labda alijiuliza:
Je, hiki kinaweza kuendesha maisha yangu?
Je, hiki kinanifanya nijisikie hai na amani kwa kjwa ninakipenda?
Je, kinanisaidia kuwa mtu wa aina gani?
Siku zote huwa natafakari na kujiuliza maswali hayo. Na sasa, kwako wewe, katika hatua yoyote ya maisha uliyonayo, tafuta muda jiulize kuhusu kazi yako:
Je, hicho unachokifanha kinaweza kuendesha maisha yako?
Je, hicho unchokifanya kinakufanya ujisikie hai, na amani na unakipenda?
Je, hicho unachokifanya kinakusaidia wewe kuwa mtu wa aina gani?
Kazi nzuri ina majibu yote matatu, hata kama kipengele kimoja kinakuwa cha kipaumbele kwa sasa. Kazi bora yenye afya zaidi kwa kawaida si pesa tupu, shauku au kitu unachopenda tupu, au ukuaji tupu. Ni muunganiko wa vyote.
Panapo majaaliwa,
Fikiri kwa kina. Ishi kwa makusudi.
Watushule

